Ramaphosa kukutana na Trump White House
21 Mei 2025Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa anakutana na Rais wa Marekani, Donald Trump katika ikulu ya White House, akiwa na lengo la kumshawishi kiongozi huyo wa Marekani kuwa na maelewano na nchi yake, badala ya kuishinikiza na kuiadhibu.
Rais Trump tangu alipoingia madarakani mwezi Januari, amekuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Ramaphosa.
Amekuwa akiiandama nchi hiyo kwa kuanzisha mageuzi ya sheria yake ya umiliki wa ardhi ambayo kimsingi yalikusudiwa kushughulikia kero ya ukosefu wa usawa na haki uliotokana na utawala wa ubaguzi wa rangi.
Ukosoaji wa Trump kwa Afrika Kusini
Trump pia amekuwa akiikosoa Afrika Kusini kwa msimamo wake wa kuifungulia kesi ya mauaji ya kimbari Israel kufuatia operesheni yake ya kijeshi katika Ukanda wa Gaza, huku akiifutia msaada na kumtimua balozi wa Afrika Kusini, mjini Washington pamoja na kuwapa hifadhi ya ukimbizi Waafrika Kusini Wazungu wa jamii ya wachache ya Afrikaans.
Ramaphosa asema yupo tayari kuzungumza na Trump kuhusu usitishaji misaada
Trump anadai watu hao wamekuwa wakiandamwa, kubaguliwa na kuuwawa. Rais Ramaphosa akiwa katika ubalozi wa nchi yake huko Washington kabla ya kwenda White House kukutana na Trump amesisitiza msimamo wa sera za taifa hilo.
"Sisi ni nchi huru yenye mamlaka yake na ni taifa tunalojivunia. Na sisi tunalinda uhuru na mamlaka yetu na siku zote tutafanya kile ambacho ni bora kwa Waafrika Kusini.''
Umuhimu wa ziara ya Ramaphosa
Ziara hii ya Ramaphosa Washington ina umuhimu mkubwa kwa Afrika Kusini, na hasa kwa kuwa Marekani ni mshirika wake nambari mbili wa kibiashara baada ya China na hatua ya Marekani ya kuikatia msaada tayari imeshaleta athari katika sekta ya afya na hasa kwenye upimaji wa maambukizi ya HIV.
Ramaphosa amesema atampa Rais Trump mapendekezo kadhaa ya makubaliano ya kibiashara.
Marekani yatishia kuufunga ubalozi mdogo wa Afrika Kusini iwapo barabara itabadilishwa jina
"Tunataka kuondoka Marekani tukiwa mkononi na makubaliano mazuri ya kibiashara, uwekezaji na uungaji mkono. Tunawekeza Marekani na Wamarekani wanawekeza kwetu. Na tunataka kuimarisha uhusiano huu na tunataka kuimarisha zaidi mahusiano kati ya mataifa yetu mawili. Kwa hivyo nina matarajio mazuri na nasubiri majadiliano.''
Ramaphosa na Trump watajadili pia masuala kuhusu siasa za kilimwengu kuanzia vita vya Israel huko Gaza hadi Ukraine. Rais Ramaphosa amesisitiza kwamba katika mazungumzo hayo atazingatia kwanza maslahi ya nchi yake na kutilia mkazo msimamo wa sera yake ya kigeni.
Miongoni mwa watakashiriki mazungumzo hayo katika ujumbe wa rais Ramaphosa ni mawaziri wake wanne huku ikitarajiwa kwamba rais Trump atakuwa pamoja na Elon Musk kwenye kikao hicho.