Ramaphosa: Uhusiano imara na US ni 'kipaumbele' kwetu
17 Machi 2025Mvutano baina ya mataifa hayo mawili ulichukua sura mpya baada ya Waziri wa Mambo ya Nje Marekani Marco Rubio kutangaza kupitia mtandao wa kijamii wa X kwamba Rasool si mtu anayetakiwa tena nchini humo akimtaja kama "mwanasiasa anayechochea ubaguzi wa rangi" pia ana chuki ya wazi dhidi ya Rais Donald Trump.
"Tunaipa kipaumbele Marekani katika uhusiano wetu wa kimataifa" alisema rais Ramaphosa mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa Marekani ni mshirika muhimu wa kibiashara kwa Afrika Kusini baada ya China.
Soma pia:Marekani yamfurusha balozi wa Afrika Kusini
Rubia alimtangaza Balozi wa Afrika kusini nchini Marekani kama mtu asiyetakiwa, baada ya Rasool kutoka maoni yake katika semina ya mtandaoni siku ya Ijumaa kwamba sera ya rais Trump ya MEGA ni itikadi ya kibaguzi na inayopinga kukuwa kwa siasa za kimaeneo.
"Tumetambua kutoridhishwa kwa Marekani dhidi ya matamshi yaliyotolewa" aliongeza rais Ramaphosa na kusisitiza kuwa Balozi Rasool atarejea Afrika Kusini na kumpa taarifa zaidi.
Rasool ambaye aliwahi kuwa mwanaharakati dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini, pia amekuwa ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Israel kuhusu vita vinavyoendelea vya Gaza.
Kuongezeka mvutano baina ya Marekani na A.Kusini
Hatua ya kumfukuza Balozi huyo inakuja katika wakati ambapo mvutano unaoongezeka kati ya Washington na Pretoria unazidi kufukuta, hasa kutokana na utofauti wa kisera, pamoja na Kesi ya Afrika Kusini dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ.
Juma lililopita Rais wa Marekani Donald Trump alizidi kuupa sura mpya mvutano huo kwa kusema kuwa wakulima wa Afrika Kusini wanakaribishwa Marekani baada ya kurudia madai kuwa serikali ya Afrika Kusini inawanyang'anya ardhi wakulima weupe. Trump ameyasema hayo bila kutoa ushahidi.
Soma pia:Kwa nini Marekani inaiadhibu Afrika Kusini kwa kuifutia misaada?
Bilionea mzaliwa wa Afrika Kusini Elon Musk, ambaye ni mshirika wa karibu wa Trump, amesema wazungu wa Afrika Kusini wamekuwa wahanga wa "sheria za umiliki wa kibaguzi."
Hata hivyo madai hayo yamepingwa na wataalam nchini Afrika Kusini, ambao wanasema hakuna ushahidi wa wazungu tu kulengwa, ingawa ni wakulima wa rangi zote ni wahasiriwa wa uvamizi wa makundi ya wahalifu katika nchi ambayo inakabiliwa na kiwango cha juu sana cha uhalifu.