Ramaphosa aufungua rasmi mkutano wa mawaziri wa fedha wa G20
26 Februari 2025Katika hotuba yake, Rais Ramaphosa amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha usawa katika upatikanaji wa fursa, hasa kwa wanawake na vijana, kama ilivyoainishwa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa. Kutoka Pretoria, Bryson Bichwa ametutumia ripoti ifuatayo. Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu wa G20 jijini Cape Town, Rais Ramaphosa alisisitiza kuwa ni muhimu kwa dunia kuungana na kuelekeza juhudi za pamoja katika kuboresha maisha ya watu, huku akitaja pia umuhimu wa kulinda vizazi vijavyo kutokana na changamoto za kijamii, kiuchumi na mazingira zinazoshuhudiwa kwa sasa. "Hatufanyi haraka vya kutosha na hata kwa ujasiri wa kutosha kukabiliana na changamoto ambazo dunia inakutana nazo. Lazima kwa pamoja tuelekeze juhudi zetu katika kuboresha maisha ya watu wa duniani, lakini muhimu zaidi, kulinda vizazi vijavyo," alisema Rais Ramaphosa.
Rais wa pia, amezungumzia umuhimu wa kuhakikisha upatikanaji sawa wa fursa kwa wote, hasa kwa wanawake na vijana, kama ilivyoainishwa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.
Amesisitiza kuwa ili mataifa yafaulu, ni lazima usawa na ustawi uwepo kwa kila mtu bila kujali jinsia, rangi, imani za kidini au hali zao za kiuchumi. "Tunahitaji kuhakikisha upatikanaji sawa wa fursa, hasa kwa wanawake na vijana, kama ilivyoainishwa wazi katika Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa. Ili mataifa yafaulu, usawa na ustawi lazima uwepo kwa kila mtu bila kujali jinsia yao, rangi yao, imani zao za kidini au hali zao za kiuchumi,"
Naye naibu Gavana wa Benki Kuu ya Afrika Kusini, Rashad Cassim, amesema moja ya changamoto kuu zinazojadiliwa kwenye huu mkutano ni jinsi ya kuchochea ukuaji wa uchumi wa dunia. Mkutano wa kwanza wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu wa kundi la G20 unaofanyika jijini Cape Town, Afrika Kusini, umefanyika bila uwepo wa baadhi ya wawakilishi kutoka nchi wanachama.
Kutokuwepo kwa baadhi ya viongozi hao kumeelezewa na wachambuzi wa masuala ya kiuchumi na diplomasia kuwa huenda kunaashiria mvutano wa kisiasa na kidiplomasia miongoni mwa mataifa wanachama, pamoja na mabadiliko ya vipaumbele vya kiuchumi kwa baadhi ya nchi.