Ramaphosa asifiwa kwa busara dhidi ya Trump
23 Mei 2025Katika moja ya matukio yaliyozua taharuki, Trump alimwonyesha Ramaphosa video yenye madai ya "mauaji ya halaiki dhidi ya wakulima wazungu" nchini Afrika Kusini – madai ambayo yamekanushwa mara kwa mara na Pretoria na ambayo wataalamu wameyaeleza kuwa ya kupotosha. Lakini licha ya mtego huo wa kisiasa, Ramaphosa alijibu kwa utulivu, na hata kumzawadia Trump kitabu kuhusu mchezo wa gofu.
Watetezi wa haki za binadamu na raia wa kawaida walitoa kauli za kuunga mkono mtindo wa Ramaphosa. Wengine walitaka majibu makali zaidi dhidi ya uongo huo, lakini wengi waliona uongozi wake kama kielelezo cha diplomasia ya kweli. “Nadhani nchi yetu imejieleza vyema na kuweka ukweli mezani,” alisema mwanaharakati Ulrich Steenkamp.
Kwa upande wa matokeo ya kisiasa, Ramaphosa alisema mkutano wao umefungua mlango kwa mazungumzo ya kina kuhusu biashara na ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili. Marekani ni mshirika wa pili kwa ukubwa wa kibiashara kwa Afrika Kusini baada ya China, na hatua ya Marekani kuashiria kuanza tena majadiliano ya biashara ilipokelewa kama mafanikio makubwa kwa Ramaphosa.
Safari ya kurejesha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili bado ni ndefu
Viongozi hao wawili walikubaliana kuongeza uwekezaji wa pande mbili, kuboresha ushirikiano wa kiteknolojia, na kushirikiana zaidi katika masuala ya ushuru na taratibu za kibiashara. Aidha, Ramaphosa alisema anaamini amemshawishi Trump kuhudhuria Mkutano wa G20 utakaofanyika Afrika Kusini mwezi Novemba mwaka huu – hatua ambayo ilikuwa ikielekea kutokuwa na matumaini kutokana na misimamo ya awali ya Marekani. Mwandishi wa shirika la habari la Associated Press, Gerald Imray, alizungumza hivi kuhusu utulivi wa Ramaphosa.
Rais Trump amshambulia Ramaphosa kwa mauaji ya wakulima wa kizungu
"Yeye huamini katika diplomasia ya upole kufanikisha mambo—mtindo wake wa kisiasa ambao ni kinyume na ule wa Trump. Ramaphosa aliutaja mkutano huo kama ushindi kwa mbinu yake ya kidiplomasia. Alisema katika mazungumzo ya faragha, ujumbe wake ulipokea zawadi za ukumbusho kutoka White House, na yeye pamoja na Trump walibadilishana zawadi—akiwemo kumpa Trump kitabu kuhusu gofu. Kwa mujibu wa Ramaphosa, hali ya baridi kati yao ilianza kuyeyuka, na kufungua njia kwa mazungumzo zaidi kuhusu biashara, ushuru, na ushirikiano wa pande mbili,"
Ramaphosa alifuatana na mawaziri wanne, wachezaji wa gofu maarufu na bilionea Johann Rupert, ambao wote walishiriki katika juhudi za kuonyesha sura halisi ya Afrika Kusini kwa utawala wa Trump. Huku baadhi ya Wamarekani wakifuatilia madai ya Trump bila kuyachuja, ujumbe wa Afrika Kusini ulijitahidi kuweka bayana kuwa matatizo ya jinai nchini humo yanawaathiri zaidi wananchi weusi kuliko wazungu, kinyume na madai ya ubaguzi dhidi ya wakulima wazungu.
Ingawa safari ya kurejesha uhusiano thabiti kati ya mataifa hayo mawili bado ni ndefu, Ramaphosa anaamini mlango sasa umefunguliwa, na msingi wa ushirikiano wa kweli umeanza kujengwa upya – kwa misingi ya ukweli, kuheshimiana, na manufaa ya pamoja.