Ramaphosa akosolewa kwa kutomfuta kazi waziri Mchunu
14 Julai 2025Wiki moja kabla ya tangazo hilo, baadhi ya raia walikuwa wakimtaka Rais Ramaphosa amchukulie hatua kali Waziri huyo anaesimamia idara ya Polisi, waliotuhumu kwa kuhujumu uhuru wa jeshi la polisi na kuvuruga misingi ya utawala wa sheria. Ili kuzuia hali hiyo isitoke nje ya mipaka, na pia kukwamisha mipango ya vyama vya upinzani kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani naye bungeni, Rais Ramaphosa siku ya Jumapili (13.07.2025), alitangaza rasmi kumpumzisha Waziri Mchunu ili kupisha uchunguzi huru.
"Ili tume iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, nimeamua kumuweka Waziri wa Polisi, Bwana Senzo Mchunu, likizo ya muda kuanzia mara moja. Waziri ameahidi kushirikiana kikamilifu na Tume ili kuiwezesha kufanya kazi yake ipasavyo," alisema Ramaphosa.
Hata hivyo, vyama vya upinzani vinasema hatua hiyo ni ya kimazoea na haina meno. Vyama kama Democratic Alliance (DA), Economic Freedom Fighters (EFF), African Transformation Movement (ATM), pamoja na Umkhonto Wesizwe (MK) vimesema Rais Ramaphosa anamlinda mshirika wake wa kisiasa kwa kumpa mapumziko yanayolipiwa badala ya kumwajibisha ipasavyo.
"Rais kwa mara nyingine ameonyesha jinsi alivyo mwoga. Ameahirisha kuchukua hatua za kweli na badala yake ameunda tume ya uchunguzi kwa kuwa hataki ionekane kama anachukua hatua dhidi ya washirika wake wa kisiasa. Na unajua, kisiasa, jinsi Mchunu alivyomsaidia katika safari yake ya kuwa rais," alisema Vuyo Zungula.
Waziri Mchunu adaiwa kuingilia utendaji wa polisi
Chanzo cha mzozo huu ni madai mazito yaliyowasilishwa na Kamishna wa Polisi wa KwaZulu-Natal, anayemtuhumu Waziri Mchunu kwa kuingilia utendaji wa polisi katika jimbo hilo kwa misingi ya kisiasa. Katika hatua ya kuonyesha mshikamano na Kamishna huyo, asasi za kiraia zinapanga kufanya maandamano ya amani kwa kuwasha mishumaa nje ya vituo vikuu vya polisi katika jimbo la Gauteng.
Mmoja wa waandamanaji, ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kama waafrika Kusini, wamechoka na kukata tamaa, akisisitiza kuwa mambo yanayoendelea ni lazima yakomeshwe na kutahadharisha serikali kuwa makini katika kuiongoza nchi.
Wachambuzi wa siasa wanasema hatua ya Rais Ramaphosa huenda ikawa ya muda tu, ikisubiri matokeo ya uchunguzi unaoendelea. Lakini kwa upande wa upinzani, shinikizo linaendelea kuongezeka kwao, likizo si suluhisho; wanataka uwajibikaji wa kweli kwa viongozi wanaotuhumiwa kuvuka mipaka ya madaraka yao.