Rais Cyril Ramaphosa aapa kutoitupa mkono Kongo
3 Februari 2025Kuuliwa kwa wanajeshi 14 wa Afrika ya Kusini huko Sake na Goma, jimboni Kivu Kaskazini kumeibua mjadala mkali nchini humo. Aidha Rais Cyril Ramaphosa amesema kufikia amani na usalama wa kudumu kwa mashariki mwa Kongo na kanda ya maziwa makuu kunahitaji utashi wa pamoja wa jumuiya ya mataifa. Ramaphosa amesisitiza kwamba Afrika Kusini haitaacha kuwaunga mkono watu wa Kongo.
Kauli ya rais wa Afrika ya Kusini imefuatia pia wapiganaji wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakuuteka mji wa Goma wiki iliyopita na kuapa kuendelea na mashambulizi yao hadi mji mkuu Kinshasa.
Ni katika mazingira hayo ndio wanajeshi 14 kutoka Afrika Kusini waliuawa. Chama cha upinzani chenye itikadi kali cha Economic Freedom Fighters (EFF) kimeitaka serikali kuwarejesha wanajeshi wao nyumbani.
Mwenye kiti wa chama cha EFF, Jilus Malema amesema kupelekwa kwa wanajeshi wa Afrika ya Kusini huko Kongo ni suala la uzembe na halikubaliki. Malema amesema ni vyema kwa Afrika Kusini iondoe wanajeshi wake ili kuhakikisha usalama wao.
Ramaphosa na shinikizo za ndani
Chama cha Democratic Alliance, ambacho kiko kwenye serikali ya mseto nchini humo, kimeomba kuweko na mjadala bungeni kuhusu kutumwa kwa wanajeshi hao. Chama hicho kilitaka kujua ni kwa nini wanajeshi wa Afrika ya Kusini walitumwa vitani bila msaada unaohitajika ikiwa ni pamoja na usaidizi wa anga.
Kwenye taarifa yake Ramaphosa alisisitiza kuwa kikosi cha kulinda amani cha Jumuiya ya SADC huko Kongo bado kinamajukumu ya kufanya na muda wake wa kuondoka. Rais Ramaphosa amesema muhula wa kikosi hicho utakamilika baada ya utekelezaji wa hatua mbalimbali za kujenga amani na pale usitishaji wa mapigano utakapotekelezwa.
Mkutano wa pamoja SADC na EAC kuhusu Kongo
Mwishoni mwa wiki iliopita marais wa Jumuiya ya SADC walitoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa kilele na marais wenzao wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kujadili njia ya kusonga mbele kuhusu hali ya usalama nchini Kongo. Marais hao pia waliahidi kuiunga mkono Kongo bila kuyumba na kusisitiza kuunga mkono juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Angola na Kenya.
Afrika Kusini inaongoza kikosi cha jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika SADC, ambacho kinakadiriwa kuwa na askari 1,300 lakini Malawi na Tanzania pia zinachangia wanajeshi. Kongo ni mwanachama wa Jumuiya ya SADC na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ikulu ya rais wa Kenya aimesema Jumattau kwamba marais wa Kongo na Rwanda wamekubali kuhudhuria mkutano wa pamoja wa kilele wa nchi wanachama wa SADC na ule wa jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Mkutano huo unapangwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania.