Rais Zelensky awasili Saudi Arabia kwa mazungumzo ya amani
11 Machi 2025Kiongozi huyo wa Ukraine aliwasili jana Jumatatu katika mji wa pwani wa Jeddah, ambapo pia anatarajiwa kukutana na mtawala wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.
Hii leo, wasuluhishi kutoka Ukraine wakiongozwa na Mkuu wa ofisi ya Rais Andrii Yermak, Waziri wa Mambo ya Nje Andrii Sybiha na Waziri wa Ulinzi Rustem Umerov watajumuika kwenye mazungumzo na ujumbe wa Marekani unaoongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio.
Zelensky hatashiriki katika mazungumzo hayo. Siku ya Jumapili alisema Kiev inatarajia matokeo yatakayosogeza suluhu ya amani na kuishawishi Marekani kuendelea kuwasaidia.
Mazungumzo hayo yanayofanyika leo Jumanne yatakuwa ni ya kwanza kati ya Ukraine na Marekani tangu vuta nikuvute iliyoshuhudiwa kwenye Ikulu ya White House kati ya Zelensky na Rais Donald Trump na Makamu wa Rais JD Vance na kupelekea Washington kusitisha msaada wa kijeshi kwa Kyiv.
Ukraine kupendekeza usitishwaji wa mapigano baharini na angani
"Tuna pendekezo la kusitishwa kwa mapigano ya angani na baharini," afisa mmoja aliiambia AFP siku ya Jumatatu, akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina. "Kwa sababu haya ndio machaguo mepesi katika kusitisha mapigano, lakini pia kufuatilia. Na upo uwezekano wa kuanza nayo."
Ukraine imekuwa ikiupinga uvamizi wa Urusi kwa msaada wa Magharibi.
Zelensky siku ya Jumatatu alisema Ukraine inataka amani, akisisitiza Urusi ndiyo "sababu pekee" ya vita hivyo.
"Ukraine imekuwa ikitafuta amani tangu sekunde ya kwanza ya vita, na kila mara tumekuwa tukisema kwamba sababu pekee ya kuendelea kwa vita ni Urusi," aliandika kwenye mtandao wa kijamii.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio siku ya Jumatatu alionyesha matumaini kabla ya mazungumzo hayo akisema anahisi kuna "matumaini". alisema hayo wakati akiwasili Jeddah na kuongeza kuwa wasingekwenda kama hawakuwa na matumaini.
Taarifa aidha zimesema, Mjumbe maalum wa Rais Trump, Steve Witkoff, anapanga kuzuru Moscow na kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin, Bloomberg na mashirika ya habari ya Reuters yaliripoti, wakinukuu vyanzo ambavyo havikutajwa, na wala havikutoa maelezo zaidi.
Witkoff, ambaye ni mjumbe rasmi wa Trump katika Mashariki ya Kati, amekuwa na mchango mkubwa katika juhudi za kumaliza vita vilivyodumu kwa miaka mitatu nchini Ukraine.
Witkoff alikutana na Putin mjini Moscow mwezi uliopitam hatua iliyopelekea kuachiliwa mwalimu raia wa Marekani Marc Fogel, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 14 katika gereza la Urusi baada ya kukamatwa akiwa na bangi aliyoandikiwa kwa ajili ya matibabu.