Xi awakaribisha 'rafiki wa enzi' Putin, Kim Jong Un Beijing
2 Septemba 2025Kwa mara ya kwanza, Rais wa China Xi Jinping amekutana hadharani na Rais wa Urusi Vladimir Putin na Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un mjini Beijing, hatua ambayo wachambuzi wanaiona kama ujumbe wa mshikamano dhidi ya mataifa ya Magharibi.
Xi alifanya mazungumzo na Putin katika Ukumbi wa Umma wa Watu na baadaye nyumbani kwake binafsi, akimuita kiongozi huyo wa Urusi "rafiki wa enzi”. Saa chache baadaye, treni ya kivita ya Kim ilishuhudiwa ikiingia Beijing, huku vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vikithibitisha kwamba kiongozi huyo alikuwa ameambatana na binti yake, Kim Ju Ae, anayechukuliwa na idara za kijasusi za Korea Kusini kama mrithi wake wa kisiasa.
Siku inayofuata, viongozi hao watatu wanatarajiwa kushiriki kwenye gwaride kubwa la kijeshi jijini Beijing, tukio litakalodhihirisha ujasiri wa Xi katika kutangaza mpangilio mpya wa dunia wakati sera za "Amerika Kwanza” za Rais Donald Trump zikivuruga mshikamano wa Magharibi.
Zaidi ya njiwa 80,000 wa amani wanatarajiwa kuachiwa angani huku maelfu wakishuhudia vifaa vya kisasa vya kijeshi vikionyeshwa kwa fahari.
Wataalamu wa masuala ya usalama wanasema ushirikiano wa karibu kati ya Beijing, Moscow na Pyongyang unaweza kubadili mizani ya nguvu za kijeshi katika eneo la Asia na Pasifiki. Hii inatokana na makubaliano ya kijeshi yaliyosainiwa kati ya Urusi na Korea Kaskazini mwaka 2024 na ushirikiano unaokua kati ya Pyongyang na Beijing.
Youngjun Kim, mchambuzi wa Taasisi ya Utafiti ya Asia ya Marekani, anabashiri kwamba mazoezi ya kijeshi ya pamoja kati ya mataifa hayo matatu "yamekaribia kuwa jambo lisiloepukika”, hali inayozitia hofu nchi za Magharibi.
Putin: Marekani inasikiliza hoja za Urusi kuhusu vita vya Ukraine
Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari akiwa Beijing, Rais Putin alisema kwamba serikali ya Rais Trump "inasikiliza hoja za Urusi” kuhusu vita vya Ukraine. Alidai kuwa sasa Moscow na Washington zimefikia "maelewano ya pamoja” kuhusu mzozo huo, ingawa hakutoa maelezo ya kina.
Hata hivyo, Trump amewahi kuonya kwamba endapo Urusi haitaonyesha ushirikiano katika juhudi za amani zinazoongozwa na Marekani, inaweza kukabiliwa na "adhabu kali”.
Wakati wa mkutano huo, kampuni ya nishati ya Urusi, Gazprom, na Shirika la Petroli la Kitaifa la China (CNPC) zilisaini makubaliano ya kuongeza kiwango cha gesi kitakachopelekwa China na kujenga bomba jipya litakalosambaza nishati kwa miaka 30 ijayo.
Hatua hii inaimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili na kuongeza hofu ya Magharibi kwamba ushirikiano huu unaweza kupunguza utegemezi wa China kwa vyanzo vya nishati kutoka nchi za Magharibi.
Kim Jong Un anatumia tukio hili kujijengea taswira ya kimataifa, hasa baada ya kupeleka zaidi ya wanajeshi 15,000 kuisaidia Urusi katika vita vya Ukraine.
Idara ya ujasusi ya Korea Kusini inaripoti kuwa karibu wanajeshi 600 wa Korea Kaskazini wameuawa katika mapigano hayo na huenda kutakuwa na duru nyingine ya wanajeshi kutumwa vitani.
Sauti dhidi ya mataifa ya Magharibi
Katika hotuba zake, Xi alishutumu kile alichokiita "ubabe wa kisiasa”, akisema kuwa dunia inahitaji mpangilio mpya wa haki na usawa. Putin naye alitetea hatua za Urusi nchini Ukraine na kulaumu mataifa ya Magharibi kwa "kuchochea mzozo” huo.
Putin alimwambia Xi kuwa uhusiano wa Urusi na China "uko katika kiwango cha kipekee kisichowahi kushuhudiwa”. Kauli hii imekuja huku mataifa hayo mawili yakiongeza ushirikiano wao wa kijeshi na kibiashara tangu Urusi iivamie Ukraine mwaka 2022, hatua ambayo imeendelea kuwasumbua washirika wa Magharibi.
Katika mkutano wa kando, Xi alikutana na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, akisisitiza kuwa China inapinga matumizi ya nguvu kutatua migogoro na inaiheshimu haki ya Iran kutumia nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia.
Kauli hii imetolewa wakati ambapo mataifa ya Ulaya yameanzisha mchakato wa kurejesha vikwazo kwa Tehran kutokana na mpango wake wa nyuklia.
Wachambuzi wanasema mshikamano huu mpya kati ya China, Urusi na Korea Kaskazini unaweza kubadilisha ramani ya usalama wa kikanda na kuipa changamoto kubwa Marekani na washirika wake.
Wakati Magharibi ikisisitiza diplomasia na mashinikizo, Beijing, Moscow na Pyongyang zinaonekana kuimarisha ushirikiano wao, zikijenga ushawishi mpya wa kisiasa, kijeshi na kiuchumi duniani.
Chanzo: rtre,dpae,afpe,Ape