Rais wa zamani wa Ujerumani Horst Köhler afariki dunia
1 Februari 2025Matangazo
Köhler aliyeiongoza Ujerumani kati ya mwaka 2004 hadi 2010, alifahamika kama muungaji mkono mkubwa wa bara la Afrika na amefariki akiwa na umri wa miaka 81.
Rais wa sasa wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amesema taifa lake limempoteza mtu muhimu aliyefanya mambo makubwa kwa nchi na dunia yote. Kansela Olaf Scholz ametuma pia salamu za rambirambi kufuatia msiba huo na amemwelezea Rais huyo wa zamani wa Ujerumani kama "mwanasiasa mwenye kujitolea aliyefanya kazi kwa ajili ya kuimarisha haki duniani.
Kabla ya kuwa rais wa Ujerumani, Horst Köhler alikuwa Mkuu wa Shirika la Fedha duniani IMF. Alishika wadhifa wa Urais baada ya kupendekezwa na kiongozi wa upinzani wa wakati huo Angela Merkel ambaye baadaye alikuwa Kansela.