Rais wa zamani wa Ufilipino Rodrigo Duterte akamatwa
11 Machi 2025Rais wa zamani wa Ufilipino Rodrigo Duterte amekamatwa leo Jumanne kwa warranti uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.
Duterte anatuhumiwa na mahakama hiyo kwa uhalifu wa kibinadamu uliotokea wakati wa kampeni yake ya kupambana na biashara na matumizi ya madawa ya kulevya wakati akiwa rais wa taifa hilo la Asia.
Rodrigo Duterte alikuwa rais wa Ufilipino kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2022 na katika utawala wake akitajwa na jumuiya ya kimataifa kuwa kiongozi aliyekiuka haki za binadamu kwa kiasi kikubwa.
Mahakama ya ICC ilikuwa ikiendesha uchunguzi kwa miaka kadhaa kuhusu mauaji ya watu wengi yaliyotokea Ufilipino chini ya utawala wake, katika kile kilichokuwa kikiitwa ni kampeini ya kukabiliana na wauza mihadharati.
Hii leo(11.03.2025) kiongozi huyo wa zamani alikamatwa akiwa uwanja wa ndege wa mjini Manila akitokea Hong Kong na kupelekwa moja kwa moja kizuizini na kuwekwa chini ya ulinzi wa dola na kukabidhiwa waranti wa kukamatwa na mwendesha mashtaka mkuu.
Kukamatwa kwake kumetokana na waranti uliotolewa na mahakama hiyo ya ICC, Machi 7.
Mahakama hiyo inamtuhumu Duterte kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, kwa mujibu wa serikali ya mjini Manila.
Tukio hilo ghafla lilizusha vurumai katika uwanja wa ndege ambako mawakili na wasaidizi wa Durtete walipiga kelele za kupinga kukamatwa kwake, pamoja na kuzuia kwa daktari na wanasheria wake kuongozana naye alikopelekwa. Silvetre Bello III ni mmoja wa mawakili wa Durtete:
"Nahisi amenyimwa haki zake za kisheria na kama rais wa zamani. Na hata ikiwa hilo linapuuzwa,lakini kwa mtu yoyote ambaye ni raia wa ufilipino unayohaki ya kupewa haki zote za kikatiba kama inavyosema katiba yetu''
Pamoja na mawakili, washirika wa kiongozi huyo wa zamani pia walisikika wakisema haki zake za kikatiba zimekiukwa.
Warranti wa ICC unasemaje
Nakala ya waranti wa ICC iliyoonekana na shirika la habari la AP, inaeleza kwamba kuna sababu za kutosha za kuamini kwamba mashambulizi dhidi ya wahanga yalienea na hata kuendeshwa kimfumo, na yalifanyika kwa miaka mingi na maelfu ya watu inaonesha waliuwawa.
Waranti huo pia umefafanuwa kwamba kuna haja ya kukamatwa kwa Duterte kuhakikisha anafikishwa mbele ya mahakama hiyo ya ICC.
Tangu kukamatwa Durtete, bado hakuna tamko la mahakama wala la ofisi ya mwendesha mashtaka wa ICC.
Familia za wahanga zashusha pumzi
Familia za wahanga waliouliwa chini ya utawala wa Durtete zimeshangilia hatua hii ya kukamatwa kiongozi huyo wa zamani huku wakisema hivi sasa wanahisi haki itapatikana sio tu dhidi ya Durtete bali hata polisi waliohusika kwenye operesheni ya mauaji.
Baadhi ya Wafilipino lakini wanasikitishwa na kukamatwa Durtete wakisema alifanya kazi nzuri nchini humo ya kutokomeza mihadarati.
Haijafahamika kiongozi huyo anashikiliwa wapi na lini atasafirishwa kupelekwa The Hague.
Ikumbukwe pia Duterte aliiondowa Ufilipino kuwa mwanachama wa ICC mwaka 2019, hatua iliyokosolewa sana wakati huo na wanaharakati wa haki za binadamu wakisema aliichukuwa kukwepa kuwajibishwa.
ICC imeshasema bado inayo mamlaka ya kisheria katika uchunguzi huu.