Buhari, Rais wa zamani wa Nigeria kuzikwa Daura
15 Julai 2025Matangazo
Maandalizi ya mazishi hayo yanaendelea huku usalama ukiwa umeimarishwa.
Askari polisi na wanajeshi kadhaa walikuwa wakiilinda nyumba yake leo mchana, huku maafisa usalama waliovalia kiraia wakionekana pia wakifanya doria.
Buhari, alifariki dunia juzi Jumapili mjini London, Uingereza, akiwa na umri wa miaka 82.
Wakaazi wa Daura wamekuwa wakielekea katika makaazi yake kwenye jimbo la Katsina kutoa heshima zao za mwisho, kabla ya mazishi hayo.
Kwa miaka kadhaa, eneo la kaskazini mwa Nigeria limekumbwa na mashambulizi ya wapiganaji wa itikadi kali na magenge ya wahalifu yenye silaha.
Ingawa alichaguliwa kwa nia ya kuleta mabadiliko, Buhari alishindwa kukomesha ghasia wakati wa utawala wake.