Rais wa zamani wa Nigeria Muhammadu Buhari aombolezwa
14 Julai 2025Taarifa iliyotolewa na rais wa sasa wa nchi hiyo Bola Tinubu, imesema kiongozi huyo amemtuma makamu wake Kashim Shettima mjini London kuratibu maandalizi na kuusindikiza mwili wa Buhari kurejeshwa Nigeria.
Rais Tinubu amesema mtangulizi wake aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa muda mrefu ambao hakuutaja.
Tinubu asifu uongozi wa Buhari
Rais huyo pia amemsifu Buhari kwa kushinikza kuwepo kwa nidhamu katika utumishi wa umma, kukabiliana moja kwa moja na ufisadi pamoja na kuiweka nchi juu ya maslahi ya kibinafsi .
Rais Tinubu, ameagiza bendera nchini humo kupeperushwa nusu mlingoti.
Lakini kwa baadhi ya wakosoaji, uongozi wa Buhari, ulishindwa kukabiliana na maovu ya muda mrefu kama vile ufisadi, umaskini na vurugu za kutumia silaha, pamoja na madai ya ukiukwaji wa haki uliotekelezwa na vikosi vya usalama.
Viongozi kadhaa wa Afrika akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Mahmoud Ali Youssouf, Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye, mkuu wa Shirika la Biashara Duniani WTO Ngozi Okonjo-Iweala, wametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Buhari huku Rais wa Africa Kusini Cyril Ramaphosa akisema kuwa uongozi wa Buhari uliyaleta karibu mataifa hayo mawili katika ushirikiano ambao umechangia ukuaji na maendeleo ya pamoja ya Afrika.
Buhari apata ushindi wa kwanza Nigeria
Buhari aliitawala Nigeria mara mbili akiwa kwanza mtawala wa kijeshi mnamo miaka ya 1980 na mnamo mwaka 2015 alichaguliwa kuwa rais kwa njia ya kidemokrasia na aliiongoza nchi hiyo kwa mara nyingine hadi mwaka 2023.