Rais wa zamani wa Kongo Joseph Kabila aitembelea Goma
28 Mei 2025Ziara hiyo inajiri mwezi mmoja baada ya kutangaza kuwa anataka kusaidia kuumaliza mzozo wa eneo hilo lililoharibiwa kwa vita. Vyanzo hivyo vitatu vimesema rais huyo wa zamani ataanza kufanya mashauriano leo na raia wa Goma, mji ulioangukia chini ya udhibiti wa M23 mnamo Januari wakati wa operesheni ambayo imeshuhudia kundi hilo likiyateka maeneo zaidi kuliko hapo awali. Watu walio karibu na Kabila walisema aliwasili Goma Jumapili usiku.
Corneille Nangaa, kiongozi wa muungano wa waasi unaojumuisha M23, pia amesema kwenye mitandao ya kijamii kwamba Kabila yuko Goma, ingawa Kabila mwenyewe hajazungumza na hakuna picha zake zilizochapishwa Goma.
Iwapo itathibitishwa, ziara hiyo inaweza kutatiza jitihada zinazoungwa mkono na Marekani za kukomesha uasi wa kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda mashariki mwa Kongo. Eneo hilo lina madini ya thamani ambayo utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump una nia ya kusaidia kuchimba.