Rais wa zamani wa Colombia atiwa hatiani kwa ufisadi
29 Julai 2025Hukumu hiyo ilitangazwa jana mjini Bogota kufutia kesi iliyofanyika kwa miezi sita, ambapo waendesha mashitaka waliwasilisha ushahidi unaoonesha kuwa rais huyo wa zamani alijaribu kuwahonga mashahidi waliomtuhumu kuwa na mafungamano na kundi moja la wanamgambo katika miaka ya 1990.
Uribe, mwenye umri wa miaka 73, anakabiliwa sasa na kifungo cha hadi miaka 12 jela, ingawa hukumu hiyo itatolewa kwenye kikao chengine cha mahakama.
Mwanasiasa huyo wa kihafidhina aliyetawala kuanzia mwaka 2002 hadi 2010 akiungwa mkono na Marekani, ni kiongozi anayependwa kwa kiwango kile kile anachochukiwa nchini Colombia, ambapo wako wanaomuona shujaa aliyeinusuru nchi yake kutoka dimbwi la machafuko na wale wanaomuhusisha na uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu na kuzuka kwa makundi ya wanamgambo wenye silaha.