Bolsonaro aagizwa kuvaa kifaa cha kufuatiliwa mguuni
18 Julai 2025Agizo hilo linatolewa baada ya polisi wa shirikisho kupekua nyumbani kwake mara mbili pamoja na makao makuu ya chama chake katika mji mkuu, Brasília, hii ikiwa ni kulingana na watu wenye ufahamu na amri ya mahakama.
Vyombo vya habari vimeripoti kwamba Bolsonaro pia amezuiliwa kutumia mitandao ya kijamii ya nchini humo ama kuwasiliana na watu wengine binafsi ambao pia wanachunguzwa na Mahakama ya Juu ya Shirikisho, ambao ni pamoja na mtoto wake wa kiume Eduardo Bolsonaro, ambaye ni wakili wa Brazil anayeishi Marekani kwa sasa na mwenye uhusiano wa karibu na Rais Donald Trump wa Marekani.
Bolsonaro anakabiliwa na kesi katika Mahakama ya Juu kwa tuhuma za kuongoza kile kinachodaiwa kuwa ni jaribio la kuandaa mapinduzi ya kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa 2022, ambao alishindwa na mpinzani wake wa mrengo wa kushoto Rais Luiz Inácio Lula da Silva.
Picha zilizorushwa na vyombo vya habari vya ndani zimeonyesha magari ya polisi yakiwa nje ya makazi ya Bolsonaro huko Brasilia.
Serikali: Ushahidi dhidi ya Bolsonaro uko wazi
Mbunge Sóstenes Cavalcante na kiongozi wa chama cha Bolsonaro kwenye baraza la wawakilishi, ameiambia Associated Press kwamba maafisa wa polisi pia walipekua ofisi ya Bolsonaro, zilizopo kwenye makao makuu ya chama.
Wakili wa Bolsonaro hakupatikana mara moja kuzungumzia hatua hiyo.
Jumanne, Mwendesha Mashtaka mkuu Paulo Gonet alisema kwenye ripoti yake mbele ya Mahakama hiyo ya Juu kwamba "ushahidi uko wazi: mshtakiwa alitenda kwa kudhamiria, wakati akiwa madarakani na baada ya kushindwa kwenye uchaguzi, kuchochea uasi, uvunjifu wa amani na utawala wa kidemokrasia wa sheria."
Bolsonaro aliitaja kesi hiyo kupitia mtandao wa X akisema inalenga "kumchafua", akiungana na rafiki yake Trump ambaye pia alilitumia neno hilo alipozuru taifa hilo na mshirika wake wa kiulinzi wa Amerika ya Kusini wiki iliyopita.
Mwenyewe Bolsonaro amesema Ijumaa kwamba hakuwahi kufikiria kutoroka nchi na kwamba mahakama ya juu kuweka hatua za tahadhari dhidi yake, ikiwa ni pamoja na kuvaa bangili ya mguuni, ni "udhalilishaji wa hali ya juu."
Majaji watano wa Mahakama hiyo ya Juu wanatarajiwa kuzichambua hatua hizo dhidi ya Bolsonaro kuanzia leo Ijumaa, Tovuti ya mahakama imearifu.