Rais wa Ujerumani ataka serikali iundwe haraka
20 Septemba 2005Berlin:
Rais Horst Köhler wa Ujerumani ameviomba vyama vya kisiasa kuharakisha kuunda serikali mpya. Amesema mjini Berlin kuwa vyama hivyo sasa vina jukumu kubwa la kutafuta suluhisho la hali hiyo ngumu. Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mazungumzo ya dharura kati ya vyama mbalimbali yataanza kesho Jumatano kati ya vyama vya SPD na Kijani. Vyama ndugu vya CDU/CSU vitaanza mazungumzo kwanza na chama cha FDP na baadaye SPD kesho kutwa Alhamisi. Undaji wa serikali mpya umekuwa mgumu kwa sababu ya matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanywa juzi Jumapili ambayo hayakutoa mshindi wala aliyeshindwa. Chama cha Kijani kimsingi kinakataa kushiriki katika serikali ya mseto ya CDU/CSU na FDP. Chama cha FDP nacho kinakataa kuungana na vyama vya SPD na Kijani. Vyama ndugu vya CDU/CSU, kwa mujibu wa matokeo rasmi, vimepata viti 225 Bungeni na Chama cha SPD kimepata viti 222. Kwa vile vyama vya CDU/CSU havina wingi mkubwa haviwezi kuunda serikali.