Rais wa Ufaransa asema taifa la Palestina litambuliwe
9 Julai 2025Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliyeko ziarani nchini Uingereza amesisitiza kutambuliwa kwa taifa la Palestina kwenye hotuba yake katika Bunge la Uingereza na kusema hiyo ndio njia pekee ya kupatikana amani katika eneo hilo la mashariki ya kati.
Macron amesema kusitisha mapigano ni suala la muda mfupi lakini kuwepo kwa suluhisho la serikali mbili kutaleta usalama wa kikanda ambao utaiwezesha Israel kuishi kwa amani na usalama pamoja na majirani zake.
Mfalme Charles III wa Uingereza amemkaribisha kiongozi huyo wa Ufaransa na wote wawili wamepongeza umuhimu wa uhusiano wa mataifa hayo mawili.
Jumatano hii, Macron ataendelea na ziara yake ambapo atakutana na Waziri Mkuu wa UingerezaKeir Starmerkwa mazungumzo yanayolenga kuisaidia Ukraine, kuongeza bajeti ya ulinzi na juhudi za pamoja za kukabiliana na wahamiaji haramu.