Rais wa Syria awasili Saudia Arabia kwa ziara ya kwanza
2 Februari 2025
Rais wa mpito wa Syria Ahmed al-Sharaa amewasili nchini Saudi Arabia leo Jumapili kwa ziara yake ya kwanza ya kimataifa tangu kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa rais wa Syria, Bashar al-Assad, vyombo vya habari vya serikali nchini humo vimeripoti.
Picha kutoka kwenye kituo cha televisheni cha serikali cha Al-Ekhbariya zimemuonesha Sharaa akilakiwa na maafisa wa Saudia Arabia.Kiongozi huyo pia ameongozana na Waziri wake wa Mambo ya nje Asaad al-Shaiban. Chombo hicho cha habari pia kimeripoti kwamba Sharaa anatazamiwa kukutana kiongozi wa Saudia, Mwanamfalme Mohammed bin Salman mjini Riyadh.
Soma zaidi. Wachunguzi wa uhalifu UN wasema Syria ina ushahidi mwingi
Sharaa, ambaye kundi lake la Kiislamu liliongoza kupinduliwa kwa Assad mwezi Disemba, aliteuliwa kuwa rais wa mpito siku ya Jumatano na Saudi Arabia ilikuwa miongoni mwa nchi ya kwanza kutuma salamu za pongezi. Mamlaka ya Syria inategemea nchi tajiri za Ghuba kufadhili ujenzi wa taifa hilo lililoharibiwa na vita na kufufua uchumi wake.