Trump kukutana na Waziri Mkuu wa Qatar
16 Julai 2025Mwandishi wa shirika la habari la Axios, Barak Ravid ameandika katika mtandao wa kijamii wa X, kwamba Trump na al-Thani watakutana Jumatano kujadiliana kuhusu mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza.
Wajumbe wa Israel na Hamas wamekuwa wakishiriki duru ya sasa ya mazungumzo hayo mjini Doha kuanzia Julai 6, wakijadili pendekezo linaloungwa mkono na Marekani la kusitisha mapigano kwa siku 60, linalolenga kuachiliwa kwa mateka na kuondoka kwa wanajeshi wa Israel, pamoja na kuumaliza mzozo huo.
Juhudi za kupatikana amani
Siku ya Jumapili, Mjumbe wa Trump katika eneo la Mashariki ya Kati, Steve Witkoff alisema ana matumaini kuhusu mazungumzo ya kusitisha mapigano yanayoendelea Qatar. Wajumbe kutoka Marekani, Qatar na Misri wamekuwa wakifanya kazi kuhakikisha makubaliano yanafikiwa.
Hata hivyo, Israel na kundi la Hamas wamegawanyika kuhusu kujiondoa kwa Israel katika eneo la Palestina. Makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano kwa miezi miwili yalimalizika wakati wa mashambulizi ya Israel yaliyowaua zaidi ya Wapalestina 400, Machi 18.
Wakati huo huo, mtaalamu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na kufuatilia hali ya mambo kwenye maeneo ya Wapalestina, Francesca Albanese amesema Israel inatekeleza "mauaji ya kimbari" katika Ukanda wa Gaza na kuzitolea wito nchi zote ulimwenguni kuchukua hatua madhubuti kuzuia mauaji hayo.
''Kila nchi inapaswa kupitia upya na kusitisha mara moja uhusiano wote na taifa la Israel. Uhusiano wa kijeshi, kimkakati, kisiasa, kidiplomasia, kiuchumi, mauzo ya bidhaa, na kuhakikisha kwamba sekta zao binafsi, bima, benki, mifuko ya pensheni, vyuo vikuu na wengine wanaotoa huduma katika mlolongo huu, wanafanya hivyo pia,'' Albanese.
Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na wajumbe kutoka mataifa 30 kwenye mji mkuu wa Colombia, Bogota, kujadili kuhusu vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas. Wajumbe hao wanatafuta njia ambazo mataifa duniani yanaweza kutumia kumaliza mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza. Mara kadhaa Israel imekuwa ikikanusha madai kwamba inafanya "mauaji ya kimbari" kwenye mzozo wa Gaza.
Wapalestina 875 wauawa karibu na vituo vya misaada Gaza
Nayo ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na haki za binaadamu, imesema Wapalestina 875 waliuawa katika wiki sita zilizopita karibu na vituo vya misaada Gaza. Wengi wa waliouawa walikuwa karibu na maeneo ya shirika la misaada linaloungwa mkono na Marekani na Israel la GHF, huku wengine 201 waliosalia wakiuawa kwenye njia za misafara ya magari yenye kutoa misaada.
Aidha, kulingana na shirika hilo Wapalestina 20 wameuawa karibu na vituo vya kugawa misaada huko Khan Younis, ambapo wengi walikufa kwa kukanyagana. Mauaji hayo yanafanyika wakati ambapo mashambulizi ya Israel yamewaua watu wengine 22, wakiwemo watoto 11.
(AFP, AP, Reuters)