Marekani yatangaza mazungumzo ya nyuklia na Iran
8 Aprili 2025Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kwamba nchi yake itafanya mazungumzo ya moja kwa moja ya ngazi ya juu na Iran juu ya mpango wa nyuklia siku ya Jumamosi. Trump ameyasema hayo katika ikulu ya Marekani White House wakati alipotembelewa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Iran imethibitisha mazungumzo hayo ambayo yamepangwa kufanyika nchini Oman ingawa yenyewe imesisitiza kwamba mazungumzo hayo hayatokuwa ya moja kwa moja.
Soma zaidi: Ukraine yaitisha mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la UN
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Tasnim, Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi atahudhuria mazungumzo hayo, pamoja na mjumbe mkuu wa Marekani katika Mashariki ya Kati, Steve Witkoff.
Katika hatua nyingine, Netanyahu na Trump wamejadili hali katika ukanda wa Gaza, ambako mpango wa usitishaji mapigano uliosimamiwa na Marekani, kati ya Israel na Hamas ulivunjika na kwamba kwa sasa mazungumzo mapya yanapangwa.