Rais Abbas awataka Hamas kuwaachia mateka wa Israel
23 Aprili 2025Akizungumza katika mkutano uliofanyika mjini Ramallah katika eneo la Ukingo wa Magharibi Abbas amesema kumaliza vita vinavyoendelea Gaza ndio kipaumbele chake, kutokana na kile alichokitaja kushuhudiwa kwa hasara kubwa, ikiwemo vifo vya raia, uharibifu wa mali kufuatia mashambulizi ya Israel katika miundombinu ya raia.
Katika hotuba yake ambayo ilichanganyika na maneno makali akiita Hamasi "wana wa mbwa" amelitaka kundi hilo kuweka silaha chini ili kuepusha vifo vya Wapalestina vinavyotokana na mashambulizi ya vikosi vya Israel, ukosefu wa huduma muhimu za kiutu, kwa kile tu alichokisema kuendelea kuwashikilia mateka wa Israel hasa akimrejelea Edan Alexander, ambaye inaripotiwa alikuwa katika orodha ya mateka ambao Israel iliomba waachiliwe katika pendekezo lililokataliwa hivi karibuni na Hamas.
"Hamas ndio wamewapa wavamizi wa kimabavu visingizio vya kuendeleza uhalifu wao katika Ukanda wa Gaza, kwa kuendelea kuwashikilia mateka." alisema.
Aliongeza kwamba "kwanini wamewachukua mateka? Mimi ndiye ninayelipa gharama, watu wetu wanalipa gharama, na wala si Israel. Hivi mmeona ni watu wangapi wamekufa tangu 2007? Kila siku tunalipa gharama. Ndugu zangu tafadhali waachilieni tu."
Kufuatia hotuba hiyo kali ya Rais wa Mamlaka ya Palestina Abbas aneyeungwa mkono na mataifa ya Magharibi na ambaye hana mamlaka juu ya Hamas, imejibiwa vikali na kundi hilo.
Soma pia:Qatar yahuzunishwa na mchakato wa mazungumzo kuhusu Gaza
Basem Naim miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu wa Hamas amesema mtu aliyetoa matamshi hayo makali "amepoteza sifa zote za uongozi."
Juhudi za upatanishi zinaendelea
Ama katika juhudi za upatanishi wa mzozo huo ziliyo chini ya Misri na Qatar, wapatanishi wanaendelea kuandaa mapendekezo ya usitishwaji wa vita kwa mwaka mmoja, kuondolewa kwa vikosi vya Israel Ukanda wa Gaza pamoja na kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa Israel. Hii ni kwa mujibu wa vyanzo kutoka ndani ya wapatanishi.
Hamas imeendelea kushikilia msimamo wake kwamba itawaachilia mateka ikiwa tu Israel itawaachilia wafungwa, itaondoa kikamilifu vikosi vyake Gaza na usitishwaji wa kudumu wa mapigano.
Soma pia:Waasi wa Huothi washambulia kwa kombora Israel
Nako katika uwanja wa mapigano Israel imeendelea kuishambulia Gaza ambapo watu 18 wameuwawa wakiwemo watu 11 waliokufa kwenye shambulizi la shule iliyogezwa kambi ya wakimbizi. Israel haijatoa tamko lolote kufuatia mashambulizi ya mapema leo.
Wakati hayo yakiendelea kundi la waasi wa Huthi nchini Yemen limethibitisha kuhusika na shambulio la kombora la mapema leo kuelekea kaskazini mwa Israel.