Rais wa China ziarani Ulaya
8 Novemba 2005Peking:
Rais wa China, Hu Jintao, leo anaanza ziara yake barani Ulaya. Kituo chake cha kwanza kitakuwa mjini London ambako atazungumza na Malkia Elizabeth wa Pili na Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair. Mazungumzo yao yatahusu kuimarisha zaidi ushirikiano wa teknolojia safi, biashara, masuala ya haki za Binaadamu katika Jamhuri ya Umma wa China na nia ya Iran na Korea ya Kaskazini ya kuwa na nishati ya kinuklia. Rais Hu atakuwa Uingereza kwa muda wa siku mbili. Kesho kutwa Alhamisi atakuwa mjini Berlin ambako amealikwa na Rais wa Ujerumani, Horst Köhler. Baadaye, ataelekea Hispania na Korea ya Kusini. Rais wa China, wakati wa ziara yake ya Ulaya, atahakikisha kuona kuwa vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya vya kutoiuzia silaha nchi yake vinaondolewa. Vikwazo hivyo vimewekwa baada ya China kukandamiza maandamano ya kupigania demokrasia katika uwanja wa Tiananmen mwaka 1989.