Rais Zelenskyy apongeza nia ya Marekani ya kuipatia msaada
14 Julai 2025Kwenye mazungumzo ambayo Zelenskyy ameyataja kuwa yalikuwa yenye manufaa, viongozi hao walijadiliana kuhusu mpango wa amani na kile wanachoweza kukifanya kwa pamoja ili hatimaye kukamilisha mchakato huo hivi karibuni. Amesema hayo kupitia ukurasa wa X.
Ushirikiano wao aidha utagusa maeneo ya kuimarisha ulinzi wa angani wa Ukraine, uzalishaji wa pamoja na manunuzi ya silaha kwa kushirikiana na Ulaya, na zaidi ya yote ni vikwazo dhidi ya Urusi ambavyo Zelenskyy amesema vinasaidia sana.
Awali Zelenskyy alinukuliwa kwenye mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Kyiv, akiishukuru Marekani kwa msaada inaoendelea kuutoa katika vita vyake dhidi ya Urusi.
"Tumekuwa na mazungumzo mazuri sana na Jenerali, na asante Jenerali kwa kuja, na asante kwa kukutana nawe mara nyingi pamoja na timu yako. Asante kwa timu yako na shukrani kwa rais kwa kuanza tena kutuletea msaada na uungwaji mkono wa vyama vyote," alisema Zelenskyy.
Pistorius aenda Marekani kuzungumzia msaada wa "Patriot"
Mbali na ziara hiyo ya Kellog, Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth mjini Washington hii leo. Pistorius anakusudia kujadilina na Hegseth suala zito la kuipa Ukraine mifumo ya ulinzi wa anga ya Patriot. Berlin, tayari imeipatia Kyiv mifumo mitatu kati ya 12 ya Patriot iliyokuwa nayo hapo awali.
Pistorius amesema alipohojiwa na gazeti la kila siku la Uingereza la The Financial Times kwamba kwa sasa wamebakiwa na mifumo sita tu. Waziri huyo wa Ulinzi wa Ujerumani aliongeza kuwa mfumo mmoja mara nyingi huwa haupatikani kutokana na matengenezo au mafunzo na imeiazima Poland mifumo miwili. Ni kwa maana hiyo basi Ujerumani haiwezi tena kutoa mifumo ya Patriot na hasa kwa kuzingatia malengo ya uwezo wa NATO wanayopaswa kuyatimiza.
Kwenye mazungumzo haya ya leo, Pistorius amesema atajadiliana na Hegseth kuhusu pendekezo lake la mwezi uliopita la Ujerumani kuinunulia Ukraine mifumo miwili ya Patriot kutoka Marekani.
Zelenskyy amuomba Svyrydenko kuwa Waziri Mkuu mpya
Tukirejea tena Kyiv, Rais Zelenskyy hii leo kwamba amemuomba Yuliia Svyrydenko kuwa Waziri Mkuu mpya, katika hatua ambayo haikutarajiwa. Svyrydenko, alikuwa akihudumu kama Naibu Waziri Mkuu wa kwanza nchini Ukraine pamoja na Waziri wa Uchumi.
Zelenskyy ameandika kwenye mtandao wa X kwamba amemuomba mwanamama huyo kuongoza serikali ya Ukraine na kuongeza kuwa anataraji kwamba atafikishiwa hivi karibuni mpango mkakati mpya wa serikali na kuongeza kuwa wamejadiliana hatua madhubuti za kuongeza uwezo wa kiuchumi wa Ukraine, kupanua programu za msaada kwa Waukraine na kuongeza uzalishaji wa ndani wa silaha.
Huyu hayo yakiendelea, ulimwengu unasubiri tangazo kubwa linalotarajiwa kutolewa na rais Trump la mkakati wake mpya wa kuipatia silaha Ukraine, huku akionyesha kutofurahishwa na hatua za Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Trump ameitoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki, huku akiahidi kupeleka mifumo muhimu ya ulinzi wa anga ya Patriot nchini Ukraine ili kuisaidia kuzuia kuongezeka kwa mashambulizi ya Urusi.