Ruto atakiwa kutuma wanajeshi Mandera kuimarisha Usalama
1 Septemba 2025Tangu vita viliporitiwa katika nchi jirani ya Somalia haswa eneo la Bula Hawa, idadi ya wakimbizi imekuwa ikiendelea kuongezeka katika jimbo la Mandera.
Kulingana na gavana wa jimbo hilo Mohamed Adan Khalif, vikosi vya Jubaland Forces vinavyopambana na jeshi la serikali ya Somalia, vimeliteka jimbo hilo na kusababisha kufungwa kwa shule ya msingi ya BP1.
Gavana Khalif amemtaka rais William Ruto kuagiza jeshi la taifa kuwafurusha wapiganaji hao nje ya nchi huku akiituhumu nchi jirani ya Ethiopia kuwaunga mkono wapiganaji waliongia Mandera.
"Majirani wetu wa Ethiopia, tunawaomba muwache kuingilia masuala ya ndani ya Mandera na Kenya. Kama mnataka kuunga mkono Somalia, mnaweza kufanya hivyo kupitia miji mingine ya mipaka yenu na Somalia”
Wakaazi katika kaunti ya Mandera wanasema, wanaishi kwa hofu kubwa kutokana na kuwepo kwa vikosi vya wanajeshi wa kigeni katika jimbo hilo liliko katika mpaka wa Kenya na Somalia.
"Tuanomba serikali watusaidie kwa kuwaondoa hawa wanjeshi hapa.tunataka tuishi maisha namna tulivyokuwa tukiishi zamani”
Kilio chao kinajiri wakati aliyekuwa naibu wa rais aliyebanduliwa Rigathi Gachagua akidai kuwa,vikosi vya Jubaland Forces vimewauawa watu watano katika jimbo la Mandera
"Haiwezekani kwamba, kuna vikosi vya kigeni katika taifa letu na serikali imekimya.Tunamuuliza kamanda wa vikosi vyote vya wanjeshi ambaye ni rais, kuagiza operesheni ya kuviondoa vikosi hivyo kutoka taifa letu”
Siku nne zilizopita, gari la serikali ya kaunti ya Mandera lilitekwa nyara na watu wasiojuikna japo dereva akanusirika.