Mahakama yazuia kikosi kazi cha Ruto
21 Agosti 2025Jaji Bahati Mwamuye wa Kitengo cha Katiba na Haki za Binadamu cha Milimani alitoa amri za muda zinazositisha utekelezaji wa Tamko la Rais lililounda Kikosi Kazi cha Pamoja cha Vita Dhidi ya Ufisadi. Kusitishwa huko ni pigo la mapema kwa Rais Ruto, ambaye mnamo Agosti 18 alikizindua kikosi hicho chenye watu 11, akikitaja kama hatua thabiti ya kuratibu na kuimarisha vita dhidi ya ufisadi kupitia mtazamo wa pamoja wa serikali nzima.
Kikosi chadaiwa kudhoofisha taasisi huru za kikatiba
Jaji Mwamuye alitoa amri hizo za muda kufuatia ombi la dharura lililowasilishwa na Dokta Magare Gikenyi, J. Benjamin, Eliud Matindi na watu wengine wawili, waliodai kwamba kikosi hicho kinadhoofisha taasisi huru za kikatiba ambazo tayari zina jukumu la kupambana na ufisadi.
Jaji aliamuru kwamba Agizo la Rais liendelee kusitishwa hadi kesi itakaposikilizwa na kuamuliwa kikamilifu.
Aliahidi kukamilisha shauri hilo ifikapo Desemba 4. Rais Ruto aliitetea hatua hiyo akisema inalenga kuhakikisha mbinu za pamoja, zenye ufanisi na matokeo dhahiri dhidi ya ufisadi, akionya kuwa ufisadi katika ofisi za serikali, ikiwemo bunge, umefikia viwango vya kutisha.
''Kuna watu wanaovuruga uadilifu wa bunge. Wanakusanya pesa kwa jina bunge."
Wakenya wadai Ruto alikiuka mamlaka yake
Kesi hiyo itatajwa na kusikilizwa kwa njia ya mtandaoni mnamo Septemba 9 ili kuthibitisha utekelezaji na kutoa mwelekeo wa usikilizaji wa haraka.
Hata hivyo, Wakenya wanadai kuwa Rais Ruto alikiuka mamlaka yake kwa kuunda kikosi hicho, wakisisitiza kuwa kinaweza kudhoofisha ofisi huru zenye jukumu la kikatiba la kuchunguza na kufuatilia ufisadi. Kuundwa kwa kikosi hicho kulifanyika siku moja baada ya Rais Ruto na kiongozi wa chama cha upinzani, ODM Raila Odinga kuwaonya wabunge dhidi ya kubadili kamati za bunge kuwa vituo vya ulaji rushwa.
Ruto aliwashutumu baadhi ya wabunge kwa kudai mamilioni ya shilingi kama hongo ili kushawishi sheria na michakato ya usimamizi, akionya kuwa wote wanaotoa na kupokea rushwa watakamatwa.
Wadadisi wanasema kwa muda mrefu, Bunge limekuwa likifanya kazi si kama nguzo huru ya serikali, bali kama muhuri wa kuidhinisha matakwa ya Ikulu. Sheria kandamizi, kodi nzito na sera zisizozingatia mahitaji ya wananchi zimepitishwa kwa pupa, mara nyingi usiku wa manane, bila mjadala wa maana.