Rais Ndayishimiye atimiza miaka mitano madarakani
18 Juni 2025Ni katika mkoa wa Gitega mji mkuu wa kisiasa na alikozaliwa ndiko rais Evariste Ndayishimiye alikojumiuika na mawaziri katika serikali yake pamoja na maafisa wakuu kutoka idara za kiserikali katika maadhimisho hayo ya mwaka wa 5 wa utawala wake.
Rais Ndayishimiye amewakumbusha maafisa hao umuhimu wa majukumu yao na kwamba ni kana kwamba wamebeba msalaba wa raia hivyo wanatakiwa kupatia jawabu kero zinazowakabili wananchi, pia kuzingatia kuwa Burundi inao utajiri wa mali asili ambapo kawahimiza kutekeleza majukumu yao kwa kuweka kipaumbele maslahi ya raia na taifa. Na kuwatahadharisha wanaoendelea kuidharau Burundi.
"Tunatakiwa kuimarisha uhuru, tuwape uhuru wananchi wote, na kulinda haki zao. Tuhakikishe kila raia anahusishwa katika maswala ya nchi. Katika desturi za warundi, raia walibadilishana fikra, ndio sababu walisema Umoja ni nguvu. Mazungumzo yamekuwa kama nembo kwa warundi", alisema Ndayishimiye.
Raia kutoka mikoa mbali mbali ya Burundi wamekuwa na maoni tafauti kuhusiana na miaka hii mitano ya utawala. Wengi wakionekana kukaribisha sera yake ya kuweka kipaumbele.
"Miaka 5 ya utawala wake ametufunza mengi, tumejuwa kuweka mashamba yetu pamoja, kumepelekea mavuno kuongezeka. Tunapata chakula na mengine tunauza na hivyo kupata pesa."
Changamoto za kiuchumi kwa raia
Baadhi ya raia wengine wanasema changamoto kiuchumi bado zimesalia tele ukilinganisha Burundi na nchi nyingine za kanda hio.
Maadhimisho hayo ya mwaka wa tano ya utawala wake yamefanyika wakati chama chake CNDD FDD kitakalia viti vyote bungeni baada ya kushinda uchaguzi wa bunge na madiwani. Muhula wa rais ikiwa ni miaka saba, utakamilika 2027 na kufanyika uchaguzi mwingine wa rais.