Rais mpya wa Syria aalikwa kwenye mkutano wa dharura Misri
24 Februari 2025Rais mpya wa Syria Ahmed al-Sharaa amepokea mwaliko kutoka kwa mwenzake wa Misri Abdel Fattah al-Sisi kuhudhuria mkutano wa dharura wa jumuiya ya nchi za kiarabu utakaofanyika mjini Cairo tarehe 4 mwezi ujao wa Machi.
Mwaliko huo unachukuliwa kuwa hatua kubwa katika kurejesha uhusiano wa Syria na mataifa ya Kiarabu baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad. EU kuondoa vikwazo katika sekta ya benki na nishati Syria
Tangu achukue madaraka, Sharaa amejitahidi kuimarisha mahusiano na mataifa ya Kiarabu, akiapa kuendesha mchakato wa mpito wa kisiasa unaojumisha kuundwa kwa serikali shirikishi na baadae kufanyika kwa uchaguzi ambao amesema unaweza kuchukua muda wa hadi miaka minne kuandaliwa.
Mkutano huo wa Cairo unatarajiwa kujikita zaidi katika juhudi za mataifa ya Kiarabu kukabiliana na mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kuugeuza ukanda wa Gaza ulioharibiwa kwa vita kuwa eneo la kimataifa la utalii, pamoja na wito wake kwa Misri na Joran kuwapa hifadhi Wapalestina waliopoteza makaazi yao.