Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuzuru Uingereza Jumanne
6 Julai 2025Ziara hiyo inalenga kuimarisha uhusiano kati ya London na Ulaya baada ya Uingereza kujiondoa rasmi katika Umoja wa Ulaya (Brexit). Macron na mkewe, Brigitte, wamealikwa na Mfalme Charles III wa Uingereza kwa ziara ya kitaifa ya siku tatu. Katika siku ya Alhamisi, Macron atafanya mazungumzo ya pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, katika Mkutano wa 37 wa Wakuu wa Ufaransa na Uingereza.Mazungumzo hayo yanatarajiwa kuangazia msaada kwa Ukraine, juhudi za pamoja za kukomesha uhamiaji haramu, na kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiulinzi kati ya mataifa hayo mawili. Kwa mujibu wa Ikulu ya Ufaransa – Elysee, hii ni ziara ya kwanza ya kitaifa kufanywa nchini Uingereza na kiongozi wa serikali ya Umoja wa Ulaya tangu kura ya maoni ya mwaka 2016 ilipoamua kujiondoa kutoka Umoja huo.