Rais wa Korea Kusini aondolewa madarakani
4 Aprili 2025Uamuzi huo uliotolewa kwa kauli moja unahitimisha miezi kadhaa ya mvutano wa kisiasa ambao umetatiza juhudi za kukabiliana na utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani, wakati huu ambapo taifa hilo la nne kwa ukubwa barani Asia linakabiliwa na kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi.
Waziri Mkuu Han Duck-soo ataendelea kuhudumu kama kaimu rais hadi kiongozi mpya atakapoapishwa ndani ya siku 60 kama inavyotakiwa na katiba.
Mahakama ilikataa hoja nyingi za Yoon ikiziita matumizi mabaya ya wingi wa wabunge, ikisema kulikuwa na njia nyingine za kisheria za kushughulikia mzozo huo.
Lee Jae-myung, kiongozi wa wengi wa chama cha kiliberali ambacho kilishindwa na Rais Yoonkwa tofauti ndogo ya kura kwenye uchaguzi wa mwaka 2022, ndiye mgombeaji mwenye nafasi nzuri ya ushindi lakini anakabiliwa na changamoto za kisheria kuhusiana na kesi nyingi za ufisadi dhidi yake. Wahafidhina wana uwezekano mkubwa wa kuwasimamisha wagombea.
Ushindi kwa demokrasia ya Korea
Kulingana na Profesa Leif-Eric Easley wa Chuo Kikuu cha Ewha huko Seoul, "Uamuzi wa pamoja wa Mahakama ya Kikatiba umeondoa chanzo kikuu cha kutokuwa na uhakika."
Amebainisha jinsi serikali ijayo ina kibarua cha kukabiliana na changamoto ikiwa ni pamoja na vitisho vya jeshi la Korea Kaskazini, shinikizo la kidiplomasia la China, na ushuru wa biashara wa Trump.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeutaja uamuzi huo kuwa ushindi kwa nchi hiyo yenye ustahimilivu, kwa juhudi zake za kutafuta haki za binadamu, na kwa maadili ya kidemokrasia.
Maelfu ya watu walioshiriki mkutano wa umma uliomtaka Yoon aondolewe madarakani walipiga mayowe ya furaha waliposikia uamuzi huo, huku wakiimba nyimbo za ushindi.
Kim Han-sol, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 23, aliyekuwa kwenye mkutano huo uliofanyika nje ya mahakama amesema "uamuzi huo ulichukua muda mrefu lakini ni bahati nzuri kwamba umetoa matokeo ya busara."
"Samahani na ninajuta sana"
Wafuasi wa Yoon walikusanyika karibu na makaazi yake rasmi wakitazama uamuzi huo kwenye runinga kubwa kwa ukimya na mshangao.
Baadhi walionesha hamaki. Mwandishi wa shirika la habari la Yonhap aliripoti kwamba mfuasi mmoja alikamatwa kwa kuvunja dirisha la basi la polisi.
Wengine walishika tama na kulia kwa uchungu lakini mikutano mingi ilifanyika kwa amani.
Kwenye ujumbe uliotolewa kupitia mawakili wake, Yoon ameomba msamaha kwa Wakorea Kusini akisema "Samahani na ninajuta sana kwamba sikuweza kutimiza matarajio yenu."
Hapo awali, mawakili wa Yoon walikuwa wameukosowa uamuzi huo wa mahakama wakiuita uamuzi wa kisiasa.
Tume ya uchaguzi ya Korea Kusini ilisema inatarajia kuwa wagombea wa urais wanaweza kuanza kujiandikisha Ijumaa, baada ya mazungumzo na kaimu Rais Han. Tarehe 3 mwezi Juni ndio inatarajiwa kuwa tarehe ya uchaguzi.