Shinikizo la kisiasa na vurugu za kidini kusini mwa Syria
17 Julai 2025Rais wa mpito wa Syria, Ahmed al-Sharaa, ameahidi kulinda haki za raia wa jamii ya Druze kufuatia kuanza kutekelezwa kwa usitishaji mapigano unaodaiwa kuungwa mkono na Marekani.
Mapigano makali yamezuka katika mji wa Sweida, makazi ya Wadruse wengi, kati ya wapiganaji wa eneo hilo, majeshi ya serikali ya Damascus na makabila ya Wabedui.
Katika hotuba yake kwa taifa, Sharaa aliishutumu Israel kwa kuchochea migawanyiko na kuvuruga uthabiti wa Syria. Hii ni baada ya Israel kufanya mashambulizi ya angani mjini Damascus na maeneo ya kusini mwa Syria ikidai inalinda maslahi ya jamii ya Druze, ambao pia ni wachache waaminifu ndani ya Israel.
Usiku wa kuamkia Alhamisi, majeshi ya serikali yaliondoka mjini Sweida, na uongozi wa kiusalama ukakabidhiwa kwa wazee wa dini na vikundi vya wenyeji. Hatua hii imeelezwa kama njia ya kuzuia nchi hiyo kutumbukia tena katika vita vikubwa baada ya miaka ya umwagaji damu iliyoisha kwa kuondolewa kwa utawala wa Bashar al-Assad Disemba mwaka jana.
Israel yaingilia kati, wasiwasi watanda
Mashambulizi ya Israel yalilenga makao ya Wizara ya Ulinzi na maeneo karibu na ikulu mjini Damascus, hatua iliyoonekana kama onyo kwa utawala mpya wa Syria. Israel ilidai kuwa haitavumilia kuwepo kwa wanamgambo wa Kiislamu karibu na mpaka wake. Jeshi lake lilihamisha brigedi kutoka Gaza hadi Ukingo wa Golan ili kujiandaa na "matukio ya aina yoyote.”
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema mashambulizi yataendelea hadi majeshi ya Syria yaondoke kabisa kusini. Maafisa wa kijeshi wa Israel wamedai wanajiandaa kuongeza mashinikizo ikiwa ujumbe wao hautasikika.
Mashirika ya haki za binadamu yameripoti vifo vya zaidi ya watu 360, wakiwemo watoto, wanawake, na askari, huku mashuhuda wakisema baadhi ya vifo vilitokea kupitia "unyongaji wa haraka." Video za mitandaoni zinaonyesha askari wa serikali wakikiuka heshima za viongozi wa kidini wa Druze.
Mgogoro wa kijamii na wasiwasi wa ndani
Wakati huo huo, wasyria wa jamii ya Druze walioko nje ya nchi wameeleza hofu kuhusu familia zao. Mwanamke mmoja kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) alisema ndugu zake walikuwa wamejificha kwenye basement wakiogopa mashambulizi. Mwingine alielezea kuwa nyumba ya jamaa zake iliteketezwa kwa moto.
Katika kisa cha kusikitisha, Evelyn Azzam kutoka Jaramana alisimulia jinsi mumewe alivyopigwa risasi na maafisa wa usalama wakati akijaribu kueleza kuwa hana uhusiano na wapiganaji. "Tangu wakati huo sijajua kilichompata,” alisema kwa huzuni.
Kwa jamii ya Druze, tukio hili linafananishwa na shambulio la Islamic State dhidi ya Sweida mwaka 2018, ambapo raia walilazimika kujihami bila msaada kutoka kwa serikali ya Assad. Hali ya sasa inaonyesha marudio ya historia hiyo ya kuachwa mkono.
Wito wa umoja na tahadhari ya kimataifa
Shirika la Syria Observatory for Human Rights limethibitisha kwamba majeshi ya serikali yameondoka kikamilifu mkoani Sweida. Badala yake, wapiganaji wa Druze wamechukua usimamizi wa kiusalama. Hatua hii ilitangazwa rasmi na Rais Sharaa ambaye alisema ni kwa "maslahi ya taifa na usalama wa pamoja."
Katika ujumbe wa video, Sharaa alisema, "Tumeamua kuwakabidhi wazee wa dini na vikundi vya wenyeji jukumu la kuimarisha usalama Sweida ili kuzuia nchi yetu isitumbukie kwenye vita vipya.” Hata hivyo, wasiwasi wa ukosefu wa uaminifu kati ya jamii za wachache na utawala mpya bado umetanda.
China imeingilia kwa kutoa wito wa kuheshimiwa kwa mamlaka ya Syria, ikikosoa mashambulizi ya Israel kama yanayoweza kuchochea mzozo mkubwa zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Hatima ya Syria: Maamuzi ya ndani au mashinikizo ya nje?
Wakati Rais Sharaa akijaribu kushona upya mshikamano wa kitaifa, changamoto ni nyingi – kuanzia wasiwasi wa jamii za wachache, shinikizo kutoka Israel, hadi ushawishi wa mataifa ya nje.
Marekani, kupitia Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, imesema imehusika moja kwa moja kufanikisha usitishaji wa mapigano na kueleza kuwa pande zote zimekubaliana juu ya hatua maalum za kurejesha utulivu.
Hata hivyo, waangalizi wanahoji iwapo makubaliano hayo yatadumu, hasa baada ya Sheikh Hikmat al-Hijri, mmoja wa viongozi mashuhuri wa Druze, kuyakataa makubaliano hayo hadharani.
Kiongozi huyo alieleza hofu ya Druze kuvutwa kwenye siasa za nje, akitaka "usalama wa kweli usimamiwe na wenyeji wenye dhamira ya amani, si wanasiasa wanaofuja damu kwa maslahi ya madaraka.”