Raila atoa wito wa mazungumzo kutuliza joto la kisasa Kenya
8 Julai 2025Wakati Wakenya walipoadhimisha miaka 35 ya maandamano ya kihistoria ya Saba Saba siku ya Jumatatu, Odinga alisema kuwa Wakenya bado wanakumbwa na changamoto zilezile zilizochochea maandamano ya mwaka 1990, ikiwemo hali ngumu ya kiuchumi na ukiukwaji wa haki za binadamu. Awali, alitarajiwa kuongoza mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kamukunji, Nairobi, lakini akaamua kuufuta kutokana na uwepo mkubwa wa polisi na vizuizi vya barabarani katika njia kuu za kuingia jiji la Nairobi.
Badala yake, kiongozi huyo wa ODM alifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo alitoa mapendekeo kadhaa ikiwemo mazungumzo ya kitaifa. Alitaja nguzo nne kuu za mazungumzo hayo ya kiraia, majadiliano kupitia mkutano wa kitaifa, Mageuzi ya polisi, Uwajibikaji na mapambano mapya dhidi ya ufisadi na uwezeshaji wa vijana na ushirikishwaji wa kiuchumi.
Watu wanne wameuawa nchini Kenya
Wakati huo huo Huduma ya Kitaifa ya Polisi NPS imethibitisha vifo vya watu 11, kukamatwa kwa watu 567 na majeruhi kadhaa wakati wa maandamano ya Saba Saba siku ya Jumatatu (07.07.2025), huku kukiwa na lawama kali dhidi ya matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Miongoni mwa waliokamatwa ni Mbunge wa Manyatta, Gitonga Mukunji, ambaye kukamatwa kwake kulitangazwa kupitia taarifa rasmi ya polisi iliyotolewa Jumatatu usiku.
Gen Z: Aliotoa amri ya vijana kupigwa risasi awajibishwe
Taarifa hiyo inaonyesha hali mbaya ya machafuko yaliyotapakaa nchini, huku mashirika ya haki za binadamu yakituhumu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi na kupuuza maagizo ya mahakama. Kulingana na NPS, maafisa wa polisi 52 na raia 11 walijeruhiwa katika mapigano yenye vurugu katika maeneo mbalimbali ya nchi. Raila amewataka Wakenya kuepuka machafuko.
“Je, tuchague machafuko au tuchague muungano wa mawazo na taifa? Mimi, nikiwa mmoja wa waasisi hai wa matukio yaliyopelekea Saba Saba, nachagua kuungana kwa mawazo na taifa kwa manufaa ya nchi yetu,” alisema Raila Odinga.
Hali ni tete mjini Nairobi huku vijana wakiendelea kushiriki maandamano ya kuipinga serikali
Maandamano hayo ya kusababisha vifo yamekuja wakati wito wa kumwajibisha Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen ukiongezeka, baada ya video kusambaa ikimuonyesha akitoa amri kwa polisi kuwapiga risasi waandamanaji endapo wangekaribia vituo vya polisi au kuonekana kuwa tishio.
Matukio haya mapya yanafikisha jumla ya vifo vinavyohusiana na maandamano kuwa angalau 39 katika kipindi cha wiki tatu, kwa mujibu wa waangalizi wa haki za binadamu.