Raia wa Zimbabwe Kirsty Coventry achaguliwa kuwa rais wa IOC
21 Machi 2025Bi Coventry, ambaye ni mshindi mara mbili wa Olimpiki katika mchezo wa kuogelea na waziri wa michezo nchini mwake Zimbabwe, aliwashangaza wengi kwa kujipatia kura 49 kati 97 zinazohitajika kushinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo na kuwapiku wagombea wengine saba.
Soma pia: Michezo ya Olimpiki kwa wenye Ulemavu yafungua pazia Paris
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 41, anarithi mikoba ya Mjerumani Thomas Bach, ambaye muda wake utamalizika baada ya miaka 12 ya uongozi.
Bach atajiuzulu Siku ya Olimpiki mnamo Juni 23 na kumpisha Kirsty Coventry atakayechukua nafasi ya rais wa 10 katika historia ya miaka 131 ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki IOC, na atahudumu muhula wa miaka minane hadi mwaka 2033, na kisha anaweza kugombea muhula mwingine mmoja wa miaka minne.