Raia wa Sudan Kaskazini washambuliwa Sudan Kusini
19 Januari 2025Hali ya wasiwasi imeendelea Sudan Kusini kufuatia mashambulizi yanayofanywa dhidi ya raia kutoka nchi jirani ya Sudan.
Watu wengine 12 wamepoteza maisha katika kipindi cha siku mbili Sudan Kusini, kwa mujibu wa ripoti za vikosi vya usalama zilizotoka Jumamosi, licha ya kutangazwa sheria ya kuwataka watu kutotoka nje usiku.
Maandamano yaliyozuka baada ya ripoti ya kuuliwa raia 29 wa Sudan Kusini katika mapigano yaliyotokea kwenye jimbo la Al Jazira nchini Sudan,yalisababisha uporoaji wa mali kwenye maduka yanayomilikiwa na raia wa Sudan katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba.
Polisi walifyetuwa risasi kuyatimuwa makundi ya watu na kuuwa watu watatu na wengine saba walijeruhiwa.
Jumamosi vikosi vya usalama vya Sudan Kusini vikasema kwamba watu 9 wameuwawa,raia wawili wa nchi hiyo na saba kutoka Sudan,wakati wa maandamano yaliyofanyika Ijumaa katika mji wa Aweil.
Siku hiyo hiyo ya Ijumaa Serikali ya Juba ikatangaza sheria ya kuwataka wananchi kutotembea nje usiku huku ikitajwa kwamba maandamano hayo yameenea hadi kwenye miji mingine.
Msemaji wa polisi John Kassara ametowa taarifa akisema hali jumla ya usalama imetulia na imedhibitiwa nchi nzima katika kipindi cha saa 24 zilizopita.Soma pia: Wakimbizi wa Sudan wateseka Sudan Kusini
Rais Salva Kiir ametowa mwito wa kuwepo utulivu katika taifa hilo. Siku ya Jumamosi mwandishi wa shirika la habari la AFP alisema mitaa ya mji mkuu Juba ilionekana ikiwa na utuluvu nyakati za jioni huku askari waliojihami kwa silaha wakiwa wamemwagwa,na maduka ya biashara yanayomilikiwa na Wasudan yakiwa bado yamefungwa.
Itakumbukwa kwamba mnamo siku ya Ijumaa raia zaidi ya 600 wa Sudan walipelekwa katika makao makuu ya jeshi la Sudan Kusini kwaajili ya ulinzi wao, huku wengine 278 wakiwemo watoto waliwekwa chini ya ulinzi wa polisi katika jimbo la Equatoria ya kati kwa mujibu wa jeshi la polisi la huko.
Kuna raia wengi wa Sudan waliokimbilia Sudan Kusini kutokana na vita katika nchi yake vilivyozuka tangu Aprili mwaka 2023. Sudan Kusini ilijitenga na jirani yake Kaskazini mwaka 2011 na imekuwa haina utulivu tangu wakati huo.