Waisraeli waandamana kushinikiza kumalizwa kwa vita Gaza
26 Agosti 2025Waandamanaji hao walizuia barabara kadhaa katika mji wa Tel Aviv huku wakipeperusha bendera za Israel na picha za mateka. Baadhi yao walikusanyika karibu na Ubalozi wa Marekani huku wengine wakiandamana nje ya nyumba za mawaziri mbalimbali.
Waandamanaji wanamtuhumu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kutoa kipaumbele katika suala la kuiangamiza Hamas kuliko kuwaachiliwa kwa mateka.
Ruby Chen, ambaye mtoto wake wa kiume alitekwa nyara na wanamgambo wa Hamas mnamo Oktoba 7, 2023 amesema Netanyahu anaona ni sawa kuwatoa mhanga mateka 50 kwa ajili ya maslahi ya kisiasa.
Mkutano wa Baraza la Usalama kufanyika
Baraza la Mawaziri la Israel linalojadili masuala ya usalama linatarajiwa baadaye leo kukutana. Hata hivyo ajenda ya mkutano haijafahamika wazi, lakini vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa huenda mada kuu ikawa ni kutathmini mchakato wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea ili kusitisha mapigano huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka.
Mapema mwezi huu, Baraza hilo liliidhinisha mpango wa kutanua operesheni za kijeshi na hatimaye kuchukua udhibiti wa mji wa Gaza, hatua iliyozusha hofu kuhusu usalama wa mateka na hivyo kuzuka wimbi jipya la maandamano ambayo yameshuhudia maelfu ya watu wakiingia mitaani huko Israel. Mpango huo umekosolewa pia vikali na jumuiya ya kimataifa.
Qatar ambayo ni mpatanishi katika mzozo huo pamoja na Misri na Marekani imesema hadi sasa "bado inasubiri" jibu la Israel kufuatia pendekezo jipya liliwasilishwa na wapatanishi na baada ya Hamas kuliafiki zaidi ya wiki moja iliyopita.
Pendekezo hilo linajumuisha usitishwaji mapigano kwa siku 60 na ubadilishanaji wa mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina lakini Israel inaonekana kusita kukubaliana na mpango huo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed al-Ansari amesema taarifa wanazozisikia hivi sasa hazitoi matumaini yoyote.
Ukosoaji waendelea kufuatia shambulio la Israel katika hospitali huko Gaza
Ukosoaji umeendelea kumiminika kufuatia shambulio la Israel katika hospitali ya al-Nasser huko Khan Younis hapo jana ambapo watu 20 waliuawa wakiwemo wanahabari watano. China imetaja kushtushwa na tukio hilo huku Umoja wa Ulaya ukilaani mashambulizi hayo. Anouar El Anouni ni msemaji wa Tume ya Umoja wa Ulaya:
" Mauaji ya waandishi wa habari watano, wahudumu wanne wa afya na idadi kadhaa ya raia huko Gaza jana kufuatia mashambulizi ya Israel hayakubaliki kabisa. Raia na waandishi wa habari wanapaswa kulindwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Kumekuwa na vifo vingi sana katika mzozo huu. Lazima vikome sasa."
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameliita shambulizi hilo kuwa la "bahati mbaya” na kusema uchunguzi umeanzishwa na kwamba Israel inajutia tukio hilo kwa kuwa inathamini kazi ya waandishi, wahudumu wa afya na raia wote.
//DPA, Reuters, AP, AFP