Qatar yaisihi Israel na Hamas kutumia “fursa”
28 Juni 2025Katika mahojiano na shirika la habari la AFP, Ansari alisema Doha, kwa kushirikiana na wapatanishi wengine kutoka Washington na Cairo, wanajaribu kutumia fursa hiyo mpya kuanzisha tena mazungumzo kuhusu Gaza. Alionya kuwa ikiwa fursa hiyo haitatumika, basi itakuwa ni nafasi nyingine muhimu iliyopotea.
Rais wa Marekani Donald Trump pia alieleza matumaini kuwa makubaliano mapya ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas yanaweza kufikiwa mapema wiki ijayo. Hata hivyo, Ansari alifafanua kuwa kwa sasa hakuna mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili, lakini Qatar inaendelea kuzungumza na kila upande kwa njia tofauti.
Mapatano ya awali ya kusitisha mapigano ya miezi miwili yaliyofikiwa Januari yalivunjika mwezi Machi, baada ya Israel kuendeleza mashambulizi makali Gaza.